WATAKAOSAIDIA WAJAWAZITO KUJIFUNGUA SALAMA KUZAWADIWA

Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, imetangaza donge nono kwa kuwazawadia fedha za motisha watoa huduma kwenye zahanati za Manispaa hiyo watakaowasaidia wajawazito kujifungua salama.
Katika hatua nyingine, Sh milioni 10.97 zimechangwa ili kuwezesha kununuliwa kwa gari la kubeba wagonjwa katika Zahanati ya Kinyerezi jijini Dar es Salaam, katika harambee iliyoendeshwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Yono Auction Mart, Scholastica Kevela juzi usiku.
Akizungumza kwenye harambee hiyo, Kaimu Mganga Mkuu wa Manispaa ya Ilala, Dk Willy Sangu alisema katika kuboresha huduma za afya, kuanzia sasa muuguzi na daktari atakayemsaidia mjamzito kujifungua salama kwenye Zahanati za Manispaa ya Ilala atapewa fedha za motisha.
“Tumechukua hatua hii kama njia ya kuwafanya wauguzi na madaktari katika zahanati zetu waweze kuwahamasisha wajawazito kupenda kujifungulia kwenye zahanati hatua itakayopunguza mlundikano wa wagonjwa katika Hospitali ya Amana.
“Kwa hiyo kwa kadri mtakavyowasaidia wajawazito kujifungua salama ndivyo kiasi cha fedha za motisha kitakavyokuwa kinaongezeka,” alisema Dk Sangu ambaye alisema kiasi cha fedha hizo za motisha kinafikia Sh 10,000 kwa kila mzazi.
Akiendesha harambee ya ununuzi wa gari la wagonjwa, Kevela ambaye pia ni Kamanda wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Kata ya Tabata Kimanga alisema mpango wa ununuzi wa gari hilo umelenga kuboresha huduma za afya katika Zahanati ya Kinyerezi.
Kevela alisema kupatikana kwa gari hilo kutarahisisha kazi ya kuwapeleka wagonjwa wanaozidiwa kwenye hospitali mbalimbali za jijini Dar es Salaam na hivyo kupunguza au kuepusha vifo visivyo vya lazima.
“Kutokana na miundombinu ya Jiji la Dar es Salaam, sisi sote tunajua umuhimu wa kuwa na gari la kubeba wagonjwa ili kuwawahisha kwenye hospitali kubwa zaidi kwa matibabu. Nimefurahi kusikia kuwa mmekusudia kununua gari hilo kabla ya kuisha kwa mwaka huu,” alisema Kevela.
Katika harambee hiyo Kevela alichangia Sh milioni 1.1, huku Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Ilala, Dk Willy Sangu akichangia Sh milioni mbili, Diwani wa Kinyerezi Leah Ng’itu alichangia Sh milioni moja na wananchi wa Kinyerezi wakiwemo watumishi wa zahanati hiyo walichangia viwango mbalimbali vya fedha ikiwa ni ahadi na fedha taslimu zilizofikia Sh milioni 10.97.

No comments: