MATOKEO UTAFITI WA CHANJO YA UKIMWI YALETA MATUMAINI



Matokeo ya utafiti wa chanjo ya ugonjwa wa Ukimwi, inayofanywa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Dar es Salaam, yameelezwa kutoa dalili nzuri, huku watu wanaofanyiwa utafiti wakifikia 198.
Ingawa utafiti huo bado unaendelea, lakini wataalamu wanaofanya utafiti huo, wamesema wana matumaini ya kupata chanjo hiyo, ingawa haijajulikana ni lini itapatikana, kutokana na kirusi hicho kubadilika mara kwa mara.
Mkuu wa Utafiti wa Chanjo ya Ukimwi kutoka chuo hicho, Profesa Muhammad Bakari aliyasema hayo wakati wa kongamano la kisayansi, lililomalizika juzi  jijini Dar es Salaam.
Alisema utafiti unaoendelea sasa ni kupata vichocheo vya kinga. Alisema utafiti huo,  ulianzia awamu ya kwanza na mpaka sasa wako awamu ya tatu, ambapo wanaangalia usalama na uwezo wa kupata vichocheo hivyo.
“Tuna matumaini makubwa ya kupata chanjo, lakini haijajulikana itapatikana lini, kwani kirusi hiki ni kijanja na utafiti kama huu unachukua muda,” alisema.
Alisema utafiti wa kwanza, ulihusisha watu 60 ambao wote walikuwa askari, awamu ya pili watu 120 na ya sasa wanayoshirikiana na wataalamu kutoka Maputo, Msumbiji inahusisha watu 198, ambao 80 kutoka Dar es Salaam, 80 Mbeya na 38 Msumbiji.
Prof Bakari alisema wanahusisha watu kutoka Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Magereza, vijana na wananchi wa kawaida.
Alisema changamoto wanayokutana nayo ni washiriki wa chanjo, wakipewa chanjo hiyo, miili inatengeneza kinga na wakipimwa kwa vipimo vya kawaida, huonekana kama wana virusi.
“Mshiriki akiambiwa ameathirika katika vituo vya kawaida, ndipo inatokea imani potofu kuwa wanapandikizwa virusi, jambo ambalo siyo kweli, kwani katika vipimo vyetu vya utafiti, vinaonesha hana virusi,” alisema.
Alisema matumaini makubwa yamepatikana kwa utafiti uliofanyika Thailand kuhusu chanjo ya Ukimwi, ambayo ina uwezo wa kukinga kwa asilimia 30. Lakini, bado ni ndogo na wanaendelea na utafiti kufikia asilimia 70.
Prof. Bakari alisema jitihada za kinga wakati zinaendelea ni vema wananchi wakaendelea kujikinga na maambukizi, kwa kubadili tabia, kwani chanjo siyo mbadala wa kupata tiba.
Alisema majaribio ya chanjo hiyo yaliyofanyika nchini mwaka 2007 mpaka 2010 na 2008 mpaka 2012, yalionesha mafanikio mazuri, ingawa hayakufikia hatua ya kupatikana kwa chanjo kamili.
Kwa mujibu wa Profesa Bakari, majaribio hayo yalithibitisha kuwa chanjo ya DNA – MVA, ilikuwa salama na yenye uwezo wa kuufanya mwili utengeneze kinga dhidi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU).
Pamoja na matokeo hayo kutia moyo, baada ya kuanza kufanya utafiti, jopo la madaktari bado liliendelea na utafiti zaidi ulioanza 2008 hadi 2012 ili kupata chanjo.
Alisema utafiti wa awali ambao ulijulikana kama HIVIS-03, ulihusisha askari 60 ambao walifuatiliwa kwa karibu wakati wote wa utafiti, ili kuhakiki usalama wa chanjo na uwezo wa chanjo kutengeneza vichocheo vya kinga dhidi ya VVU.

No comments: