JESHI LA POLISI LILICHANGIA ASKARI 192 ULINZI NJE YA NCHIJeshi la Polisi lilichangia jumla ya askari 192 walioshiriki ulinzi wa amani nje ya nchi katika nchi za Sudan, Sudan Kusini na Lebanon.
Hayo yalisema bungeni na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chakawe wakati akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2014/2015.
Alisema kati ya askari hao 181 walikuwa Sudan, watano Sudani Kusini na sita Lebanon na kwa mwaka 2014/2015 Jeshi la Polisi litaendelea kuwaruhusu maofisa, wakaguzi na askari kufanya mitihani maalumu inayowawezesha kushiriki katika operesheni za ulinzi wa amani ndani na nje ya nchi.
Alisema katika kipindi cha  Julai 2013 hadi Machi 2014, wageni 113 walipatiwa uraia.
Pia katika kipindi cha Julai 2013 hadi Machi 2014, Watanzania 35 waliukana uraia wa Tanzana kwa sababu mbalimbali na kupata uraia wa mataifa mengine idadi yao ikiwa kwenye mabano ni Ujerumani (6), Denmark (6), Namibia (6), Norway (9), Uingereza (3) na mmoja mmoja katika nchi za Bulgaria, Botswana, Afrika Kusini na Marekani, hivyo watu hao kupoteza sifa ya kuwa raia wa Tanzania.
Aidha katika kipindi hicho Watanzania `wazamiaji’ 605 walirudishwa nchini kutoka nchi mbalimbali, hususan Afrika Kusini.
Alisema  kati ya Julai hadi Desemba  2013, taarifa za wananchi na doria za Jeshi la Polisi zimewezesha kukamatwa kwa jumla ya kilo 221,898 za dawa za kulevya za viwandani, ambazo ni heroin, kokeni, bangi na mandrax.
Watuhumiwa 905 walikamatwa na kufikishwa mahakamani pia kilo 265,576,545 za bangi na kilo 16,822,305 za mirungi zilikamatwa na watuhumiwa 14,284 walikamatwa na kufikishwa mahakamani. Pia jumla ya hekta 580.5 za mashamba ya bangi ziliteketezwa.
Pia, alisema katika mwaka 2013/2014 mamlaka ya vitambulisho vya taifa imekamilisha usajili kwa wakazi 560,297 wa Unguja na Pemba na wakazi 2,449,822 wa mkoa wa Dar es Salaam, hivyo idadi yote ya waliosajiliwa ni 3,300,119, ambapo wakazi hao wote watapatiwa vitambulisho vya taifa.
Waziri Chikawe alisema katika kipindi mwaka 2013/2014 kumekuwepo na migogoro mbalimbali ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji, wakulima wakitaka kumiliki ardhi kwa ajili ya kilimo wakati wafugaji nao wakiitaka ardhi hiyo.
Alisema migogoro hiyo ilitokea katika maeneo ya Hanang, Kiteto, Mvomero, Kondoa, Singida na Mbeya, ambapo ilisababisha mapigano baina ya makundi hayo na kusababisha watu 47 kujeruhiwa na 16 kuuawa.
Aidha migogoro hiyo ilisababisha vifo vya watu na majeruhi 20 mwaka 2012/2013 na ilitokea katika mikoa ya Tanga, Pwani, Mbeya, Morogoro na Arusha.

No comments: