Hifadhi ya Jamii ni haki ya kila mtu
nchini katika kumhakikishia usalama wa upatikanaji wa masuala yote ya msingi
pindi dharura zinapotokea.
Hayo yalisemwa na Mjumbe wa Menejimenti
na Mkuu wa Ununuzi wa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya
Jamii nchini (SSRA), Emmanuel Urembo wakati wa
semina ya juu ya shughuli na majukumu ya mamlaka hiyo, iliyofanyika
mjini hapa juzi.
Urembo alisema haki hiyo imeainishwa
vizuri katika Katiba ya nchi na kwenye Sera ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii ya
mwaka 2003..
Alisema Taifa lina wajibu wa kuhakikisha
kuwa kiwango cha chini cha maisha kwa kila mwananchi kinafikiwa, kwa kumpatia
kila mtu mambo yote ya msingi ya kijamii bila kujali hali ya kipato, michango
au ajira yake.
Aidha, alisema sheria iliyounda SSRA
inaruhusu uandikishaji wa wanachama kutoka sekta isiyokuwa rasmi, mfano
wakulima na wafanyabiashara ndogo, kuwa na haki ya kujiunga kwenye mfumo wa
ziada.
Kwa mujibu wa Urembo, wananchi wapatao
milioni moja na nusu walio kwenye sekta rasmi tu nchini, ndio wanaonufaika na
Hifadhi ya Jamii, jambo ambalo ni changamoto kubwa kwa mamlaka hiyo.
Changamoto nyingine ni pamoja na mfumo
uliopo hivi sasa kutoruhusu mwanachama mmoja kuhamia Mfuko mwingine, kuwepo kwa
tofauti kubwa kwenye fomula za ukokotoaji wa mafao na tofauti ya mafao kuwa
kubwa kati ya Mfuko mmoja na mwingine.
No comments:
Post a Comment