MAMIA WAJITOKEZA KUAGA MWILI WA BALOZI WA MALAWIMakamu wa Rais Dk Mohamed Gharib Bilal, jana aliongoza mamia ya wananchi wakiwamo viongozi wa Serikali, mabalozi wa nchi mbalimbali na wanataaluma, kuuaga mwili wa Balozi wa Malawi nchini, Flossie Chiyaonga.
Mbali na Makamu wa Rais wengine waliohudhuria misa ya kuagwa kwa balozi huyo ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Asha Rose Migiro na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, John haule.
Awali, mwili wa marehemu uliingizwa katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) na baadae kufuatiwa na misa iliyoendeshwa na Mchungaji Peterson Muridhi wa Kanisa la St Columbas la Upanga, aliyetokea nchini Kenya.
Akizungumza katika ukumbi huo, Waziri Membe alisema kifo cha Balozi Chiyaonga kimewagusa watu wengi kutokana na kuwa cha ghafla bila kutegemewa.
Alisema alikuwa akitekeleza majukumu yake ipasavyo kwa kusaidia kuboresha uhusiano baina ya nchi mbili ya Tanzania na Malawi, hivyo kuondoka kwake ni pengo kubwa kwa nchi zote mbili.
"Alikuwa mtu mzuri sana, ataishi milele tutamkumbuka daima lakini ataendelea kuwa nasi daima na siku moja tutakutana. Huu mshituko tumepata wote, tunashirikiana katika majonzi na maumivu katika kipindi hiki kigumu," alisema Waziri Membe.
Alisema mara zote Balozi Chiyaonga alikuwa akimsisitiza kuhakikisha kuwaunganisha watu wa Tanzania na Malawi kuwa wamoja. Pia kuendeleza mazuri aliyofanya Balozi Chiyaonga.
Mwakilishi wa Ubalozi wa Malawi, Kwacha Chisiza alisema kifo cha Balozi huyo ni pigo kubwa kwa serikali zote na kuishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuonesha umoja wao na kutoa ndege   ya kusafirisha mwili wa marehemu. Waziri Membe anatarajiwa kuondoka leo pamoja na mwili wa marehemu.
Balozi Flossie alifariki Ijumaa iliyopita wakati akipelekwa katika Hospitali ya Aga Khan kwa matibabu, baada ya kuugua akiwa nyumbani kwake.

Jumatatu iliyopita usiku, Balozi Flossie alijisikia vibaya na kupelekwa Aga Khan, ambako alipatiwa matibabu na kuwekwa mapumziko kati ya saa sita usiku na saa 12 asubuhi, ambapo alipatiwa dawa za kutumia nyumbani na kuruhusiwa.
Kwa mujibu wa Haule, hali ilibadilika mchana na kurejeshwa hospitalini  lakini alipofikishwa Aga Khan, madaktari walimfanyia vipimo na kubaini ameshafariki.
Alisema wakati wa uhai wake, Balozi Flossie alifanya kazi zake kwa kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na Malawi na kushirikiana vizuri na mabalozi wenzake wanaowakilisha nchi zao Tanzania.

No comments: