MPANGO WA KUSHUSHA GHARAMA ZA UMEME WASITISHWASerikali imetangaza na kusisitiza mpango wake wa kupunguza bei ya umeme kwa wananchi, utakaoanza mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara mpaka Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stephen Masele, alisema hayo jana bungeni, alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Martha Mlata (CCM).
Martha katika swali lake Mlata aliitaka Serikali kupunguza bei ya umeme, ili wananchi wa kawaida watumie nishati hiyo kupikia  na kupunguza matumizi ya mkaa yanayochangia kuharibu mazingira nchini.
Akifafanua zaidi, Masele aliwataka Watanzania kuvuta subira kwa kuwa ujenzi wa bomba hilo kwa sasa umefikia kati ya asilimia 80 na 90 kukamilika na ukikamilika, utawezesha kupungua kwa bei ya umeme.
Kwa mujibu wa Masele, kwa sasa Shirika la Umeme (Tanesco), linanunua umeme kutoka katika kampuni za ufuaji umeme wa mafuta kwa senti 38 na 55 za dola za Marekani kwa uniti moja, ili kuwauzia Watanzania.
Wakati kampuni hizo zikiuza umeme kwa bei hiyo, takwimu za Tanesco zinaonesha kuwa shirika hilo linalazimika kuuza umeme huo kwa kati ya senti 10 mpaka senti 19 za dola za Marekani kwa uniti moja kwa wananchi.
Takwimu hizo zinaonesha kuwa wateja wa majumbani uniti moja ya umeme wanauziwa kwa senti 19 za dola za Marekani, wateja wa biashara senti 13, viwanda vya kati na vikubwa senti 10 na taa za barabarani senti 19. 
Kwa takwimu hizo na kwa bei hizo, Tanesco katika kila uniti moja ya umeme inayouza imekuwa ikipata hasara ya senti 28 mpaka 36 za dola za Marekani.
Katika mpango wa Serikali, Masele alisema bomba hilo likianza kufanya kazi, umeme utaanza kununuliwa na Tanesco kutoka kwa wafanyabiashara kwa kati ya senti nane hadi tisa za dola za Marekani tofauti na sasa ambapo umeme unanunuliwa kwa kati ya Dola 38 na 55.
Alifafanua kwamba baada ya kuanza kununua umeme kwa bei nafuu, Serikali inapanga kupunguza bei ya umeme katika muda usiozidi miezi 12.
Masele alitangaza hayo bungeni huku kukiwa na taarifa kuwa wafanyabiashara wanaouzia umeme Tanesco, wamekuwa wakipambana bei hiyo isishuke.
Wafanyabiashara hao wenye mitambo ya kufua umeme wa mafuta na waagizaji wa mafuta, wanafanya jitihada kuhakikisha lengo hilo halifikiwi, kwa kuwa watapoteza karibu Sh bilioni nne wanazopata kila siku kutoka Tanesco.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda, alipokuwa mkoani Mtwara kukagua ujenzi wa bomba la gesi hivi karibuni alisema kuwa wafanyabiashara hao wako katika mapambano kutaka malengo ya kushusha bei ya umeme yasifikiwe.
“Sisi tunaona kuwa suluhu ya kuondokana na gharama hizi (za umeme) ni gesi, lakini kuna watu wanajua watanyang’anywa tonge mdomoni, vita hii tunaijua; lakini sisi hatuwezi kurudi nyuma katika hili ni lazima tuendelee mbele,” alisema Pinda.
Pinda alisema mapambano hayo yalianza tangu wakati wa jaribio la kuzuia gesi isifike Dar es Salaam, kwa kuwa wafanyabiashara hao wanahofia kuwa mwisho wa biashara yao ya kuuzia Tanesco umeme kwa bei ya juu, umefika. 
Alisisitiza kuwa Serikali imedhamiria kuachana na umeme huo wa mafuta na kama wafanyabiashara hao wanataka kuendelea na biashara hiyo, ni vyema wabadilishe mitambo yao iwe ya gesi na sio ya mafuta kama ilivyo sasa hivi.

No comments: