MAPATO YA ZANZIBAR KWENYE MUUNGANO YAWEKWA HADHARANI



Fedha zinazopelekwa Zanzibar kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa ajili ya kusaidia shughuli mbalimbali  za kibajeti, kiuchumi na kijamii, zimewekwa wazi ambapo miongoni mwake zipo zinazotokana na Malipo ya Kodi ya Mishahara (Paye).
Wakati Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano, Samia Suluhu Hassan aliwasilisha taarifa hiyo jana bungeni, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, ilisema kutofahamika kwa fedha zinazopelekwa Zanzibar kutoka Serikali ya  Muungano, kunachangia baadhi  ya watu kubeza Muungano.
Waziri Samia alitoa taarifa hiyo wakati wa kuwasilisha  makadirio ya Bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2014/15.
Alisema kuanzia Julai Mosi, 2013 hadi Machi 31 mwaka huu, Sh bilioni 15.75 za Paye zimemepokewa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).
Fedha hizo za Paye kwa mujibu wa Waziri, ni matokeo ya makubaliano kati mawaziri wa SMZ na wa Muungano baada ya kuwepo madai ya Zanzibar kutaka kupata fungu kutokana na mapato hayo kwa wafanyakazi wa taasisi za Muungano wanaofanya kazi Zanzibar.
“Hata hivyo marekebisho ya kisheria hususani Sheria ya Kodi ya Mapato  (Paye) yanahitajika ili kuweka utaratibu wa wazi,” alisema Samia.
Licha ya Paye, gawio lingine kwa SMZ ni linalojumuisha asilimia 4.5 ya misaada ya kibajeti. Alisema hadi Machi mwaka huu, SMZ imepata msaada wa kibajeti wa Sh bilioni 27.19 kati ya Sh bilioni 32.62 zilizoidhinishwa na Bunge kwa mwaka wa fedha 2013/14.
Aidha katika kipindi cha kuanzia, fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo zilizopelekwa Zanzibar ni Sh bilioni 1.24. Vile vile Serikali ya Muungano ilichangia Sh milioni 600 kwenda SMZ kwa ajili ya kufanikisha maadhimisho ya miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Vile vile Waziri alisema katika kipindi hiki, masuala ya kijamii yameratibiwa na kunufaisha wananchi wa pande zote za Muungano.
“Serikali zetu kwa ushirikiano zimeendelea kubuni na kutekeleza miradi mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wake.”  
Alitaja miradi hiyo inayofadhiliwa na Serikali kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo. Baadhi ya miradi hiyo ni pamoja na Mradi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (Tasaf), Mradi wa Maendeleo ya Sekta ya Kilimo (ASDP), Mradi wa Maendeleo ya Mifugo (ASDP-L) na Millennium  Challenge Account Tanzania (MCA). 
Katika mwaka wa fedha 2014/15, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano imeomba Bunge liidhinishe Sh bilioni 5.7 kwa ajili ya matumizi ya kawaida. Kiasi hicho kinajumuisha fedha za mishahara Sh milioni 879.5 na fedha za matumizi mengineyo Sh bilioni 4.84.

No comments: