Serikali imesema
kuanzia sasa itawaondoa madarakani mameya, wenyeviti wa halmashauri na
wakurugenzi katika halmashauri zitakazokumbwa na mgogoro.
Waziri Mkuu
Mizengo Pinda, alisema mjini hapa jana kuwa hatua hiyo inalenga kuwafanya
viongozi wa halmashauri za wilaya nchini, kutumia muda mwingi katika kutekeleza
miradi ya maendeleo, ili kuwaletea maendeleo wananchi.
Pinda aliyekuwa
akifungua rasmi Mkutano Mkuu wa 30 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa (ALAT),
unaokwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 30 ya jumuiya hiyo, alisema tayari
amemuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia kuangalia namna ya kuanza kutekeleza agizo hilo.
Alisema kutokana
na ubinafsi wa baadhi ya mameya, halmashauri zimekuwa zikitumbukia kwenye
migogoro ya ajabu ajabu isiyo na tija wala maana kwa wananchi, hatua ambayo
imekuwa ikisababisha mipango ya maendeleo kuzorota.
Kwa mujibu wa
Pinda, kutokana na sababu mbalimbali Serikali imekuwa ikichukua hatua za
kuwafukuza kazi wakurugenzi wa halmashauri kama njia ya kukuza nidhamu na
uwajibikaji, ambapo alisema tayari wakurugenzi watano wamefukuzwa kazi.
“Ni vizuri sasa
kila panapozuka tofauti katika maeneo yenu, mjenge mazoea ya kukaa chini na
kujadili tofauti hizo ili kuzimaliza. Katika kila jambo mtakalokaa chini na
kulijadili kwa muda mrefu, iwe ni kwa ajili ya kuwasaidia wananchi na si
vinginevyo.
“Nchi yetu ina
matatizo makubwa, ipo migogoro ya wakulima na wafugaji na ipo migogoro ya
kidini pia. Tumieni muda mwingi kujadili jinsi ya kuondoa matatizo haya,
tumieni wazee katika maeneo yenu kuyamaliza haya ili tupate muda mwingi zaidi
wa kuwaletea wananchi maendeleo,” alisema Pinda.
Akitolea mfano
wa mgogoro unaosababishwa na ubinafsi, Pinda alisema aliyekuwa Meya wa
Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba, Anatory Amani, ameshindwa kuangalia maslahi
ya wananchi walio wengi na kung’ang’ania madaraka hayo, hatua inayofanya
halmashauri hiyo kushindwa kufanya vikao vya kupitisha bajeti na kupanga
mipango ya maendeleo.
“Suala hili la
mgogoro wa Bukoba sijalipenda hata kidogo. Mgogoro huu wa Bukoba ni wa kipuuzi.
Tulimtuma CAG (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Ludovick Utouh) akagundua
madudu ya ovyo mengi.
“Kwa kuona hali
ilivyo tulimshauri Meya yule ajiuzulu
kwa maana sasa fedha hazisimamiwi, hakuna vikao. Kwanza alikubali na
katika kikao akasema ameona ajiuzulu, watu wakashangilia pale na nikaletewa
barua ya kujiuzulu kwake na mimi nikaipitisha kukubali.
“Lakini baada ya
siku tatu madiwani wanaomuunga mkono, wakakimbilia mahakamani kuzuia kufanyika
kwa vikao vyovyote na Hakimu akawakubalia. Sasa kuna mradi wa kuboresha Mji wa
Bukoba wa thamani ya Sh bilioni 17, ulikuwa ufanyike lakini nao umekwama na
fedha hizo sasa zitarudi zilikotoka.
“Sasa huu ni
ubinafsi wa hali ya juu sana, yaani Meya unafikia hatua unaangalia maslahi yako
binafsi na si maslahi ya wananchi. Mbele ya maslahi ya umma wewe mtu mmoja si
chochote. Suala la kujiuzulu ni suala la baraka kwa Mungu maana leo wewe
mtu mmoja upo na kesho haupo,” alisema.
Awali Mwenyekiti
wa ALAT Taifa, Dk Didas Massaburi, alimueleza Waziri Mkuu mafanikio
yaliyofikiwa katika kuboresha maisha ya wananchi katika ngazi za Serikali
za Mitaa, huku akisema mafanikio hayo yameelekezwa katika ugatuaji wa fedha
kwenda katika serikali za mitaa, ugatuaji wa rasilimali watu, uboreshaji wa
uhusiano baina ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa na pia kuwajengea uwezo
madiwani katika kutekeleza majukumu yao.
No comments:
Post a Comment