NHC YATAKA ARDHI IJENGE NYUMBA ZA BEI NAFUUWakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya, Manispaa, Miji na Majiji wamehamasishwa kulipatia Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), ardhi ili liweze kujenga nyumba za bei nafuu na kuwauzia wananchi wa maeneo hayo.
Mwito huo ulitolewa jana na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara wa NHC, David Shambwe wakati wa Maonesho ya 30 ya Jumuiya ya Tawala za Mitaa (ALAT) yanayoendelea mjini hapa.      
Shirika la Nyumba la Taifa ni miongoni mwa wafadhili wa mkutano huo mkuu wa 30 wa ALAT  huku wafadhili wakuu wakiwa ni Benki ya NMB. Mbali yao Daily News na Habarileo pia wanafadhili mkutano huo.
Shambwe alisema Shirika la NHC lipo katika utekelezaji wa Mpango Mkakati wa ujenzi wa nyumba 15,000 za bei nafuu katika maeneo mbalimbali nchini chini ya kaulimbiu ya Nyumba Yangu Maisha Yangu kwa lengo la kuwafanya wananchi kuzingatia kwamba umiliki wa nyumba bora ni sehemu ya maisha yao.
Alisema chini ya mpango huo, NHC itajenga nyumba katika maeneo ya Ilembo mkoani Katavi,  Unyankumi mkoani Singida, Mkuzo mkoani Ruvuma, Kongwa mkoani Dodoma, Bombambili mkoani Geita, Mlole mkoani Kigoma, Mkinga mkoani Tanga, Mvomero mkoani Morogoro, Mrara mkoani Manyara na Mtanda mkoani Lindi.                                                                       
“Haya ni maeneo ambayo NHC itajenga nyumba hizi bora na za bei nafuu ili kuwawezesha wafanyakazi, wakulima na wananchi wa kawaida kuzinunua na kuishi maisha mazuri,”  alisema.
 Shambwe ambaye pia alisema mfanyakazi anaweza kukopeshwa baada ya kutoa asilimia 10 ya gharama halisi na fedha zinazobaki akalipa kwa muda utakaopangwa. Alisema Wilaya ya Mvomero imekuwa ya mfano baada ya kununua nyumba 10 zilizojengwa na NHC kwa matumizi ya watumishi wake, hatua itakayowafanya kuhamasika kufanya kazi kwa bidii kutokana na kuishi katika makazi bora na kuzitaka halmashauri nyingine nchini kuiga mfano huo.

No comments: