MAHAKAMA YAAHIDI KUONDOA MLUNDIKANO WA KESIJaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Othman Chande, amesema Mahakama imejipanga kuondoa tatizo la mlundikano wa mashauri ya muda mrefu ndani ya miezi18 ijayo.
Kauli hiyo aliitoa jana katika ufunguzi wa mkutano wa Baraza la Mahakama uliofanyika mjini hapa.
Alisema mashauri hayo yako mahakamani kwa zaidi ya miaka miwili na kuendelea na lengo ni kuondoa tatizo hilo ambalo limekuwa likilalamikiwa na wananchi wengi.
Jaji Chande alisema Mahakama imeamua kufanya kazi kwa malengo na vipimo kwa kumaliza mashauri kwa wakati.
Alisema sasa kila Mahakama imeainisha kesi zote za muda mrefu za zaidi ya miaka miwili; “tunataka miezi 18 ijayo kesi ziondoke na kutolewa hukumu.”
Jaji Chande alisema Mahakama imejipanga kuhakikisha  kuna kuwa na upatikanaji wa taarifa kwa wakati na  taarifa hizo zitakuwa zikikusanywa kila baada ya wiki mbili.
Alisema Mahakama imejipanga kuweka usimamizi na ufuatiliaji kwa mwaka ujao kuanzia ngazi ya chini hadi ya juu, ambapo kabla ya Bajeti ijayo, mikoa takribani nane itapatiwa magari kwa ajili ya kufanya ukaguzi katika mahakama mbalimbali kuangalia mienendo ya mashauri.
 “Mafanikio ni mengi lakini ni lazima tuwe na malengo katika kuboresha utendaji kazi wa kila siku ili kuhakikisha hatua inapigwa,” alisema.

No comments: