TIC KUENDELEA KUSAIDIA WAJASIRIAMALI



Kituo cha Uwekezaji (TIC) kitaendelea kusaidia wajasiriamali wadogo, kujenga uwezo katika biashara zao, ili wakue na kukuza uchumi wao na wa nchi kwa ujumla.
Mkurugenzi wa Huduma wa kituo hicho, Nakuala Senzia, ameyasema hayo hivi karibuni, wakati wa kufunga mafunzo ya siku sita ya wajasiriamali wadogo 27, wanaojishughulisha na ufugaji wa ng’ombe wa maziwa kutoka mikoa ya Pwani, Morogoro na Tanga.
“Mafunzo haya ni mwanzo tu wa kukuza wafugaji hawa ili waendelee kuuza maziwa kwa ufanisi zaidi,” alisema huku akikitaja kiwanda cha Tanga Fresh Ltd, kuwa ni soko ambalo wafugaji hao wanaweza kuuza maziwa yao.  
Alisisitiza kuwa kituo hicho kitaendelea kushirikiana na uongozi wa Mkoa wa Tanga na  wadau wengine,  kuhakikisha wanawakuza wajasiriamali wadogo pamoja na kutangaza shughuli za uwekezaji katika mkoa huo.
“Mkoa wa Tanga una fursa nyingi, hivyo ni jukumu letu kushirikiana na taasisi nyingine kukuza wajasiriamali hawa na kutangaza uwekezaji katika jiji hili,” alisisitiza.
Aliongeza kuwa moja ya majukumu makubwa kwa sasa ni kuhakikisha wajasiriamali wadogo wanakuwa katika kila kona ya nchi, ili kupunguza wimbi la utegemezi katika jamii na kuhakikisha fursa za uwekezaji zinatangazwa ndani na nje ya nchi.
“TIC ni taasisi za Serikali ambayo inatambua uwepo wa wajasiriamali wadogo na tunatambua kuwa wanahitaji kukuza kibiashara na kwa kufanya hivi tunatimiza azma ya Serikali katika kuwainua watu wetu,” aliongeza.
Aliishukuru kampuni ya Tanga Fresh Ltd, kwa kusimamia   uratibu hadi kupatikana wajasiriamali 27 na kuwaingiza katika programu hiyo ya mafunzo, yanayoendeshwa kwa ushirikiano baina ya TIC na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Maendeleo na Biashara (UNCTAD).
Katibu Tawala wa Wilaya ya Tanga, Marcelline Patrice, alisema TIC na Tanga Fresh Ltd wamefungua milango ya mafanikio kwa wajasiriamali wa wilaya yake pamoja na mikoa jirani iliyoshiriki katika mafunzo hayo.
“Muwe makini katika kufanya biashara zenu, naamini sasa mtakua mmeiva kwa muda mliokaa hapa,” aliwaambia washiriki hao.
Aliwataka wajasiriamali hao kutokuwa waoga  kuchukua mikopo katika taasisi za fedha, kwani hiyo ndio njia ya  kuwainua katika biashara zao.
“Wajasiriamali wengi wamekua waoga kuingia katika taasisi za fedha…waende huko kukopa, ndio mwanzo wa kukua kibiashara,” aliongeza.
Mmoja kati ya wajasiriamali waliopewa mafunzo hayo,   Beatrice Chanika, alielezea mafunzo hayo kuwa ni mkombozi mkubwa katika shughuli zao za ufugaji. “TIC waendelee kutusaidia ili tukue,” alisema Beatrice.

No comments: