DOLA YAOMBWA KUSAMBARATISHA UGAIDI NCHINITume ya Kikristo ya Huduma za Jamii (CSSC), imeomba Serikali kutumia dola kusambaratisha mtandao wa ugaidi,  ambao umekuwa ukilipua makanisa  na maeneo yake.
Katika tamko hilo, Tume hiyo ilitaja  tukio la wiki iliyopita, ambapo bomu lililipuka katika hosteli iliyo katika eneo la Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT),  inayomilikiwa na kanisa hilo na kujeruhi mhudumu.
Akizungumza jana katika eneo kulipolipuka bomu hilo, Mwenyekiti wa Tume hiyo,  Kanda ya Ziwa Askofu Benson Bagonza,  alisema Serikali inayo nguvu ya kutosha kuangamiza mtandao huo.
Alisema mtandao huo umekuwa ukikosesha amani kutokana na matukio ya kigaidi yanayofanywa na baadhi ya watu kwa kupigwa na mabomu, kumwagiwa tindikali pamoja na makanisa kuchomwa moto.
“Tamko letu haliko kwa ajili ya kumtuhumu mtu yeyote kuhusika na tukio hili na sisi kama Watanzania tuendelee kuwa kitu kimoja,” alisema.
Alitaka Serikali isikubali kuendelea kuchezewa na mipaka ya nchi iwe salama kwa ulinzi kwani yaweza kuwa waliofanya tukio hilo ni watu wa ndani ya nchi au nje ya nchi, ili uhuru wa kukusanyika na kuabudu uwepo bila kujali itikadi za kidini.
Askofu Irene Nzwalla wa Kanisa la Hossana Mwanza alisema kupitia maombi Mungu atamfichua mhusika wa tukio hilo, ikiwa waumini watashirikiana katika maombi, kwani tukio hilo sio la Kanisa la KKKT  pekee,  bali ni la Wakristo wote.
Hata hivyo  Askofu wa KKKT, Dayosisi Mashariki ya Ziwa Victoria, Andrew Gulla alisema hali ya majeruhi Bernadetha Alfred ambaye amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando inaendelea vizuri baada ya
kufanyiwa upasuaji.

No comments: