TIGO YAJA NA NJIA RAHISI ZAIDI YA KUTUMA NA KUPOKEA PESAKampuni ya simu za mikononi ya Tigo Tanzania, imezindua huduma mpya ya kutuma na kupokea fedha kwa njia rahisi na ya ufanisi zaidi kwa wateja wenye simu zenye programu aina ya android na iOS, ambayo ni huduma ya kwanza ya aina hiyo Afrika Mashariki.
Mkuu wa Huduma za kifedha wa Tigo, Andrew Hodgson alisema Dar es Salaam jana kuwa kuanzia sasa watumiaji wa simu za kisasa za smartphones nchini, wataweza kufanya miamala yoyote ya Tigo Pesa, ikiwemo kulipia huduma na bidhaa.
“Unaweza kutuma fedha kupitia benki, na kuongeza salio kwa uharaka na urahisi zaidi kwa kutumia ‘Tigo Pesa Application’, unaweza ukaona namba zote za simu zilizohifadhiwa katika simu yako wakati wa kuchagua kutuma fedha kupitia huduma hii ya ‘Tigo Pesa App’,” alisema Hodgson.
Alisema pia mtumiaji wa simu hizo anaweza kuhifadhi kumbukumbu za malipo yake pamoja na miamala ya kibenki aliyoifanya kwa ajili ya kuipata kiurahisi kama itahitajika maelezo yake siku za karibuni.
Hodgson alisema katika huduma hiyo, mteja ataweza kupata huduma ya Tigo Pesa katika mtandao wa Tigo bila kuingia gharama yoyote ya data, na kwamba wataweza kutumia akaunti zao za Tigo Pesa popote pale walipo duniani kupitia intaneti ya Wi-Fi au mtandao wowote uliopo wa intaneti kupitia simu kama amesajiliwa na Tigo Pesa.
Wiki mbili zilizopita, Tigo ilitoa huduma ya Facebook bure kwa wateja wake, jambo linaloelezwa na Hodgson kuwa ni moja ya utekelezaji wa dira ya kampuni ya Tigo katika kuendeleza ubunifu na huduma ambazo ni rahisi kutumia na zinazowafurahisha wateja wake.

No comments: