MADAKTARI BINGWA KUTOKA INDIA WAJA NCHINIMadaktari bingwa wa viungo na mgongo kutoka India, wanatarajia kuwasili nchini wiki hii kwa ajili ya kuwachunguza na kutibu watu wenye maradhi hayo.
Taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Hospitali ya Regency, Dk Rajni Kanabar  ilisema madaktari hao, wataendesha kambi ya siku mbili kuanzia Mei 17 mwaka huu.
Iliwataja wataalamu hao kuwa ni Dk Dipak Deva na Dk Ronak Desai, ambao ni wataalamu wa mgongo na viungo. Mwingine ni Dk Hemang Baxi, ambaye ni mtaalamu wa vibofu vya mkojo na saratani. Mtaalamu mwingine ni Dk Jignesh Patel na Dk Tarum Dave, ambao ni wataalamu wa maradhi ya moyo.
Ilisema kambi ya uchunguzi wa maradhi hayo, imeandaliwa kwa pamoja na Klabu ya Lions ya Dar es Salaam na Hospitali ya Regency.
Taarifa hiyo iliwataka watu wenye maradhi hayo, kutumia fursa hiyo kupata matibabu kutoka kwa wataalamu hao.
“Ujio wa wataalamu hawa ni fursa nzuri kwa watu wenye maradhi ya aina hii, kwani Watanzania wengi hawawezi kumudu kwenda India kutibiwa, sasa watumie fursa hii kuwaona madaktari hawa wakiwa hapa hapa nchini,” ilisema taarifa hiyo.

No comments: