WANAFUNZI BAGAMOYO WAHIMIZWA KUZINGATIA MASOMOWanafunzi wa shule za sekondari wilayani Bagamoyo, wametakiwa kusoma kwa bidii na kufanya vizuri kwenye mitihani yao, kama wanataka kufanikiwa katika maisha yao, kwani elimu ni mkombozi wa maisha ya binadamu.
Mwito huo umetolewa hivi karibuni na Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (Wama), Mama Salma  Kikwete, wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wanafunzi wa shule za sekondari za Mandera na Mboga wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.
Mama Kikwete ambaye pia ni mke wa Rais Jakaya  Kikwete, alisema kama wanafunzi hao watasoma na kufanya vizuri katika mitihani yao, watafanikiwa  kimaisha, watapata kazi na  kuwasaidia ndugu zao na  kupunguza tatizo la umasikini ndani ya jamii zao. 
“Mjenge tabia ya kusoma kwa makundi, msione fahari kukaa nyumbani hasa mwisho wa wiki, tumieni muda wenu wa ziada kusoma kwa pamoja, mchague viongozi wa makundi na kila mmoja wenu awe na somo la kuwafundisha wenzake hii itasaidia kila mtu kufaidika  na  mwenzake,” alisema Mama Kikwete.
Mwenyekiti huyo wa Wama aliwaasa wanafunzi wa kike, kutokubali kudanganywa na wanaume na kujiingiza katika uhusiano wa kimapenzi wangali wanafunzi, kwani kufanya hivyo watapata mimba zisizotarajiwa na ugonjwa wa Ukimwi, hivyo kukatisha masomo yao na kutotimiza ndoto zao.
 “Msikubali kudanyanywa na wanaume na kujiingiza katika uhusiano wa kimapenzi wakati uko shule, hata kama mzazi wako hana fedha za kutosha za kukupatia, usikimbilie kwa mwanamume.
“Unaweza kutumia kipindi cha likizo kufuga kuku wa asili na unaporudi shuleni unawaomba walezi wako wakuangalizie kuku hao wakikua utawauza na kujipatia fedha,” alisema.
Kwa upande wa walimu, aliwata kulea wanafunzi hao kama watoto wao wa kuwazaa kwani wao ndiyo wenye dhamana kubwa katika malezi ya wanafunzi.

No comments: