MABEHEWA MAPYA YA TRENI KUANZA KUINGIA JULAI

Mabehewa mapya 22 ya abiria, 274 ya mizigo na 34 ya breki pamoja na vichwa vinane vipya vya treni, yanatarajiwa kuwasili kati ya Julai na Desemba mwaka huu, imefahamika.
Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe alitangaza hayo bungeni juzi usiku wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2014/15.
Dk Mwakyembe alisema mkataba wa ununuzi wa vichwa vya treni 13 ulisainiwa Aprili, 2013 na malipo yote yamefanyika na vichwa hivyo vinatarajiwa kuanza kuwasili nchini Desemba mwaka huu.
“Ununuzi wa mabehewa mapya 22 ya abiria mkataba ulisainiwa Machi, 2013 na malipo yote yamefanyika. Mabehewa hayo yanatarajiwa kuanza kuwasili nchini mwishoni mwa Septemba, 2014,” alisema Dk Mwakyembe.
Kuhusu ununuzi wa mabehewa 274 ya mizigo, alisema mkataba ulisainiwa Machi, 2013, na malipo ya awali yalikamilika Februari, 2014 na malipo ya mwisho yanatarajiwa kukamilika kabla ya mwisho wa Juni 2014, na mabehewa hayo yataanza kuwasili nchini Septemba, 2014.
“Ununuzi wa mabehewa 25 ya kubebea kokoto. Malipo yote yamekamilika na mabehewa hayo yanatarajiwa kuanza kuwasili nchini Julai, 2014,” alifafanua Dk Mwakyembe ambaye leo Bunge litajadili makadirio hayo, kabla ya kuamua kuyapitisha.
Alisema katika mwaka 2013/14, utendaji wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) haukufikia kiwango kilichotarajiwa kutokana na hali ya miundombinu na vifaa vya uendeshaji. Ilisafirisha tani 154,341 za mizigo mwaka jana ikilinganishwa na tani 198,024 mwaka 2012.
Kuhusu TAZARA, alisema Serikali imeshatoa Sh bilioni 5.87 kwa ajili ya malipo ya wastaafu na Sh bilioni 4.69 kwa ajili ya kuongeza mtaji.

No comments: