PINDA ATAKA UFUMBUZI UHABA WA MADAWATI

Waziri Mkuu Mizengo Pinda ameutaka uongozi wa Mkoa wa Rukwa uhakikishe unamaliza tatizo la upungufu wa madawati ili watoto wa shule za msingi wasiendelee kukaa chini.
Alitoa agizo hilo juzi usiku wakati akizungumza na viongozi na watendaji wa Mkoa wa Rukwa mara baada ya kupokea taarifa ya Mkoa huo, Ikulu ndogo, mjini Sumbawanga.
Waziri Mkuu aliwasili mkoani Rukwa juzi jioni akitokea Dodoma ambapo alimwakilisha Rais Jakaya Kikwete kwenye Ibada ya kumuweka wakfu Askofu Mteule Conrad Nguvumali wa Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Rukwa iliyofanyika jana kwenye Uwanja wa Nelson Mandela, mjini Sumbawanga.
Akifafanua kuhusu tatizo la madawati, Waziri Mkuu alisema: “Lazima mjipange kama Mkoa ili muweze kusaidia juhudi za Serikali kupunguza tatizo la madawati kwa watoto wetu wa shule za msingi.
“Lazima mje na mpango maalumu… mathalani kwenye Halmashauri zenu huko, angalieni hizo mbao zinazokamatwa. Badala ya kuziuza, hizo mbao ziende kutengeneza madawati na yakikamilika yaamuliwe kabisa haya yanakwenda shule fulani, na utaratibu uendelee hadi shule zimalizike,” aliongeza.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka idara za elimu za Mkoa wa Rukwa, Halmashauri tatu za wilaya za Mkoa huo ambazo ni Nkasi, Kalambo na Sumbawanga Vijijini zinakabiliwa na upungufu wa madawati 33,799, wakati mahitaji ya madawati ni 62,118 na yaliyopo ni 28,319. Manispaa ya Sumbawanga ilisema ina upungufu wa madawati 675 bila kutaja yaliyopo ni mangapi wala mahitaji yake ni kiasi gani.

No comments: