MAASKOFU WAMTABIRIA MAKUBWA KIGWANGALA



Maaskofu wa Kanisa la Pentekoste Zanzibar, wamemsifu Mbunge wa Nzega, Dk Hamis Kigwangala kuwa ni kiongozi anayejali Muungano na kumtabiria makubwa katika safari yake ya kisiasa nchini. 
Viongozi hao wa dini, walisema hayo juzi wakati  wa Tamasha la Amani na uzinduzi wa albamu ya Jiwe ni Jiwe ya Kwaya ya Tumaini ya Kanisa la Pentekoste Tanzania (FPCT).
Tamasha hilo lilifanyika kwenye Ukumbi wa CCM Mkoa wa Mjini Magharibi, ambako Dk Kigwangala alikuwa mgeni rasmi. 
Askofu wa Kanisa  la Tanzania Assemblies of God (TAG), Dk Dickson Kaganga, akimkaribisha Mbunge Kigwangala alisema kitendo cha Mbunge huyo kukubali mwaliko wa kuwa mgeni rasmi katika tamasha hilo Zanzibar, kinaonesha jinsi alivyo muumini wa Muungano. 
“Umetoka mbali sana kule Nzega, umevuka maji hadi huku Zanzibar, umeonesha upendo sana na kwa sababu kuna amani, tunashukuru Mungu kwa kukufikisha salama.
Kwa kitendo hiki cha upendo, tunakutabiria makubwa siku za usoni na tunakuombea kwa Mungu akufanikishie,” alisema Askofu Kaganga, maarufu Mzee wa Viwango na Uwiano. 
Akizungumza katika tamasha hilo, Kigwangala aliwataka waumini wa madhehebu mbalimbali nchini, kuendeleza amani iliyopo kwa kuwa imetokana na uimara wa Muungano wa nchi mbili, ambao umedumu kwa nusu karne sasa.
Alisema wako watu, hawapendi kuwepo kwa Muungano na kuwataka Watanzania wasiwape nafasi ya kuuvunja. 
Dk Kigwangala alisema siku zote, waumini wa dini mbalimbali wanapenda amani na kuonya kuwa kama amani ikitoweka, italeta mfarakano. 
Alisema ametoka Tanzania Bara kwenda kuzindua Tamasha hilo Zanzibar, kutokana kuwepo kwa Muungano, ulioasisiwa na Mwalimu Julius Nyerere wa Tanganyika na Shekhe Abeid Amaan Karume wa Zanzibar. 
Katika tamasha hilo, Mbunge huyo alinunua albamu tatu kwa Sh 1,000,000 kuunga mkono mafanikio ya Kwaya ya Tumaini ya kanisa hilo.

No comments: