KESI YA MBUNGE WA BAHI YAPIGWA KALENDAUamuzi wa ombi la Mbunge wa Bahi, Omary Badwell (CCM),  kwamba usikilizwaji wa kesi inayomkabili ya kuomba na kupokea rushwa ya Sh milioni nane usitishwe, utatolewa Mei 12 mwaka huu. 
Uamuzi huo ulipaswa kutolewa jana na Hakimu Mkazi Hellen Riwa, lakini iliahirishwa kwa sababu Hakimu huyo ana udhuru.
Badwell aliomba kesi hiyo isiendelee kusikilizwa, kwa kuwa amefungua kesi ya kikatiba Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kuhoji kifungu cha sheria kinachokataza mshitakiwa katika kesi za jinai kukata rufani.  
Kupitia kwa Wakili wake Mpare Mpoki, Badwell alidai wamefungua kesi hiyo kwa kuwa kifungu hicho kinapingana na Ibara ya 13(6)(a) ya Katiba, ambayo inampa haki mtu yeyote kupinga uamuzi wowote ambao anaona utamuathiri.
Aidha anaiomba Mahakama Kuu itamke kifungu hicho ni batili na kinapingana na Katiba kwa kuwa Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya kikatiba. 
Wakili Mpoki alidai wakiendelea kusikiliza kesi hiyo, wataendelea kuvunja haki ya mshitakiwa, ambayo tayari ilishavunjwa na kuomba kesi hiyo isimamishwe hadi watakapopata uamuzi wa Mahakama Kuu.
Katika kesi ya msingi, inadaiwa kati ya Mei 30 na Juni 2 mwaka 2012, katika maeneo tofauti Dar es Salaam, mshitakiwa alishawishi apewe rushwa ya Sh milioni nane kutoka kwa aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, Sipora Liana.
Ilidaiwa kwamba Badwel aliomba rushwa hiyo ili awashawishi wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), kupitisha hesabu za Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani. Pia anadaiwa Juni 2, 2012 katika Hoteli ya Peacock, iliyopo Ilala, alipokea rushwa ya Sh milioni moja kutoka kwa Sipora.

No comments: