KESI YA WACHINA WA MENO YA TEMBO KUSIKILIZWA MEI 13Mashahidi wa upande wa mashitaka katika kesi ya kukutwa na meno ya tembo yenye thamani ya Sh bilioni 5.4, inayowakabili raia watatu wa China, wataendelea kutoa ushahidi Mei 13 na 14 mwaka huu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Washitakiwa hao ni Huang Gin (50), Xu Fujie (22) na Chen Jinzhan (31), wote wakazi wa eneo la Mikocheni B, Barabara ya Kifaru, Dar es Salaam.
Wakili wa Serikali, Faraja Nchimbi alidai jana mbele ya Hakimu Mfawidhi  Isaya Arufani, kuwa kesi hiyo imekuja kwa kutajwa na kuomba tarehe nyingine ya kuendelea kusikilizwa.
Hakimu Arufani aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 13 na 14 mwaka huu, watakapoendelea kusikiliza ushahidi wa upande wa mashitaka.
Hivi karibuni mahakama hiyo, ilitoa amri kwa waandishi wa habari, kutoandika mashahidi wa upande wa mashitaka kwa ajili ya usalama wao.
Alidai kuwa Novemba 2, mwaka jana katika mtaa wa Kifaru Mikocheni B, washitakiwa walikamatwa wakiwa na vipande 706 vya meno ya tembo vyenye uzito wa kilo 1,889 vyote vikiwa na thamani hiyo, mali ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bila kuwa na kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Alidai katika mashitaka mengine, wanadaiwa kutaka kutoa rushwa ya Sh milioni 30.2 kwa askari Polisi na askari wa Wanyamapori ili wasifunguliwe mashitaka.
Katika mashitaka mengine, washitakiwa wanadaiwa siku hiyo hiyo walikutwa na ganda la risasi bila kuwa na kibali cha kumiliki silaha. Washitakiwa hao walikana mashitaka yao na kurudishwa rumande hadi Februari 17 mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena.

No comments: