MGEJA ADAI LEMBELI AMELEWA MADARAKAMwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja amedai kuwa kauli ya Mbunge wa Jimbo la Kahama, James Lembeli ya kusema kuwa CCM si mama yake ni kama kitendo cha kulewa madaraka aliyokuwa nayo.
Mgeja alitoa kauli hiyo wakati akiwahutubia wakazi wa kata ya  Isaka katika ziara yake ya kuzungumzia maendeleo, amani na upendo na kukagua shughuli za maendeleo, kama Ilani ya CCM inavyoahidi.
Alisema wao kama Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Shinyanga, wamekuwa wakipokea simu mbalimbali kutoka kwa wadau, kulaani kauli hiyo iliyosemwa na Mbunge huyo, tena mbele ya vyombo vya habari.
Aidha, Mwenyekiti huyo alisema CCM ndiyo imemfikisha Mbunge huyo alipo na kimemfanya hadi kupata fursa za kutembelea hadi nchi za nje, lakini kauli yake hiyo,  haileti tija kwa chama hicho ambacho hadi hivi sasa ni Mbunge kupitia CCM.
 “Sisi hatuna tabu juu ya mambo mengine yanayomhusu yeye, kama kuunga mkono serikali tatu, lakini sisi kama wanachama wa CCM Mkoa wa Shinyanga tunapingana na kauli yake moja tu ya kusema CCM si mama yake,” alisema Mgeja na kuongeza;
 “Leo katika mkutano huu, sina nafasi ya kuzungumzia kauli ya Mbunge huyu, kwani Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Mkoa alishasema haya awali na kutuwakilisha uongozi wa Mkoa wa Shinyanga katika kulaani kitendo cha  Mbunge huyu wa CCM” alisema.
Pia, Mgeja aliwataka Watanzania kuunga mkono mfumo wa serikali mbili katika mchakato wa kupata Katiba mpya.
Aliwataka viongozi wa matawi ya CCM, kuwaambia wananchi wao faida za serikali mbili, badala ya kushabikia serikali tatu, kama walivyo wabunge wa upinzani.
Mwenyekiti huyo wa CCM wa Mkoa alisema kitendo cha viongozi kupenda serikali tatu ni kama kitendo cha kuwabebesha Watanzania mzigo.

No comments: