KIKWETE AUNDA TUME OPERESHENI TOKOMEZA

Rais Jakaya Kikwete ameunda Tume ya Uchunguzi  wa vitendo vilivyotokana na uendeshaji wa Operesheni Tokomeza.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Dar es Salaam na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, Rais ameunda tume hiyo kwa mujibu wa Kifungu cha tatu cha Sheria ya Uchunguzi Sura ya 32.
Kutokana na hatua ya kuunda tume hiyo, Rais Kikwete amemteua Jaji na Balozi mstaafu Hamisi Msumi kuwa Mwenyekiti wa Tume hiyo.
Aidha, Rais Kikwete amewateua  Jaji mstaafu Stephen Ihema na Jaji mstaafu Vincent  Lyimo kuwa Makamishna. Rais pia amemteua  Frederick Manyanda, Wakili wa Serikali katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwa Katibu wa Tume hiyo. Taarifa ya Balozi Sefue ilisema kuwa uteuzi huo ulianza juzi.
Majukumu ya tume hiyo yameelezwa kuwa ni  kuchunguza na kubaini Operesheni Tokomeza ilivyoendeshwa, kuchunguza na kubaini iwapo Sheria, Kanuni, Taratibu na Hadidu za Rejea zilifuatwa na watu waliotekeleza Operesheni Tokomeza na kuchunguza na kubaini iwapo yupo mtu yeyote aliyekiuka sheria, taratibu na hadidu za rejea wakati wa operesheni hiyo.
Aidha itachunguza na kubaini kama wapo watu waliokiuka sheria yoyote wakati wa utekelezaji wa operesheni hiyo na kupima kama hatua zilizochukuliwa dhidi yao au mali zao, zilikuwa stahiki.
Tume hiyo pia itapendekeza hatua zozote, zinazopaswa kuchukuliwa dhidi ya mtu yeyote, atakayebainika kukiuka sheria, taratibu na hadidu za rejea za Operesheni Tokomeza.
Pia, itapendekeza mambo ya kuzingatiwa wakati wa kuandaa na kutekeleza operesheni nyingine siku zijazo ili kuepuka kasoro.
Uteuzi huo wa tume hiyo, unatekeleza ahadi ya Rais Kikwete, ambayo aliitoa wakati alipohutubia Bunge Novemba 18, mwaka jana mjini Dodoma.

No comments: