MAMA AFUNGWA KWA 'KUMBAMBIKIA' MWANAUME MTOTO

Mahakama ya Mwanzo  Old Shinyanga  katika Manispaa ya Shinyanga, imemhukumu Pendo Joachim (33) mkazi wa kijiji hicho, kutumikia kifungo cha nje  cha mwaka mmoja  na kutakiwa kulipa faini ya Sh milioni moja.
Amepewa adhabu hiyo baada ya kupatikana na kosa la kusingizia mtoto kwa mwanamume mwingine ili apate pesa za matumizi.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu wa Mahakama  hiyo,  Christian Chovenye alisema Mahakama imemtia hatiani mwanamke huyo kwa kosa la udanganyifu, ambapo Deus Njile alikuwa akimhudumia mtoto huyo kwa miaka mitatu mfululizo,  akijua kuwa mtoto  ni wake.
Katika maelezo yake, Njile alidai kuwa alibaini  kuwa mtoto huyo si wake, baada ya kuona kadi mbili za kliniki, zenye majina tofauti ya baba. Baada ya kubaini hali hiyo, aliamua kwenda kwenye  uongozi wa kijiji ili apate suluhu juu ya mtoto huyo.
Ilidaiwa kuwa mbele ya Uongozi wa Kijiji, mwanamke huyo alikiri kuwa mtoto ni wa mwanamume mwingine na alifanya hivyo ili apate huduma ya mtoto.
Hata hivyo, Njile hakuishia hapo bali alipofungua kesi katika Mahakama ya Mwanzo ya Old Shinyanga, kwa madai ya kusingiziwa mtoto na kumhudumia kwa miaka mitatu.
Njile alitaka Mahakama iamuru alipwe fidia ya fedha, alizomhudumia mtoto huyo. Kesi  hiyo ilifunguliwa Machi 9, mwaka huu na hukumu ilitolewa Aprili 30, mwaka huu.
Mshitakiwa alipotakiwa kujitetea, aliiomba Mahakama impunguzie adhabu kwa sababu ana watoto wawili, wanaomtegemea. Pia, alidai yeye ni mgonjwa wa shinikizo la damu.  Mahakama ilimtaka alipe fedha hizo, Sh milioni moja ndani ya miezi kumi na mbili.

No comments: