KIBUKU YAZINDUA BIDHAA MPYA


Kampuni ya Dar Brew maarufu zaidi kama Kibuku, imezindua rasmi bia mpya ya asili ya ‘Kibuku Super’, iliyowekwa katika chupa maalumu, ambayo mteja anaweza kuondoka nayo.Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa Dar Brew, Kirowi Suma, alisema wanaingiza bidhaa hiyo mpya sokoni iliyo na ubora wa hali ya juu, huku ikiwa na uwezo wa kukaa sokoni kwa muda mrefu zaidi. 
Suma alisema kinywaji hicho kitauzwa kwa Sh 1,200 kikiwa na ujazo wa lita moja na hakina kemikali yoyote, kwani kimetengenezwa kwa kimea halisi mtumiaji hatapata mzio baada ya kutumia. 
“Leo (jana) ni siku ya furaha kubwa kwetu Dar Brew na kwa watumiaji wote wa bia, tumeingiza sokoni kinywaji kipya cha Kibuku Super ambacho kinatarajiwa kuleta mapinduzi makubwa katika soko la bia hapa nchini.
“Bia hii imetengenezwa kwa utaalamu wa hali ya juu na kwa kutumia mitambo ya kisasa kabisa ili kuwahakikishia wanywaji ubora wa hali ya juu,” alisema Suma.
Alisema, bia hiyo inatengenezwa kwa kutumia malighafi za Tanzania, ikiwemo nafaka ya mtama ulio bora toka kwenye ardhi yetu na kutaka Watanzania kujivunia kilicho cha na kukumbuka asili yao.“Kibuku Super ina kilevi cha asilimia 4, kinachokufanya uweze kuitumia kwa muda mrefu ukiwa na marafiki, lakini pia inakupa lishe nzuri kutokana na virutubisho vinavyopatikana katika nafaka zinazotumika kutengeneza bia hii.
“Kwa sasa bia hii itaanza kupatikana katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro na Dodoma, kisha itaenea nchi nzima,” alisema.Akizungumzia juu ya usambazaji, Meneja Mauzo wa Dar Brew, Saidi Mremi, alisema Kibuku Super itaanza kupatikana leo katika baa zote, maduka makubwa na sehemu nyinginezo zinazouza vileo.“Tuna imani kubwa wapenzi wa bia wataipokea bia hii mpya kwa shangwe na furaha watatumia bia hii kuonesha kuwa wanajali asili yao,” alisemaUzinduzi huo ulihudhuriwa na wafanyakazi wa kiwanda hicho kilichopo Ubungo, wauzaji wa jumla na rejareja na wageni wengi waalikwa.

No comments: