KESI YA MADABIDA YAAHIRISHWA HADI JUNI 10Kesi ya kusambaza dawa bandia za kupunguza makali ya Ukimwi (ARVs), inayomkabili Ofisa Mtendaji Mkuu wa kiwanda cha Tanzania Pharmacetical Ltd ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhan Madabida na wenzake, imeahirishwa hadi Juni 10 mwaka huu.
Jana kesi hiyo ilitajwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa ajili ya kuwasomea washitakiwa maelezo ya awali, lakini Hakimu Mkazi Nyigulila aliahirisha kwasabu ya kwenda kwenye msiba.
Alidai anaahirisha kesi hiyo hadi Juni 10 kwa kuwa wanakwenda kwenye mazishi ya daktari bingwa wa magonjwa ya akili, Gilbert Buberwa aliyefariki kwa ugonjwa wa dengue.
Mbali na kushitakiwa kwa kusambaza dawa hizo, Madabida na wenzake wanadaiwa kusababisha hasara ya Sh milioni 148 baada ya kusambaza dawa hizo kupitia kiwanda chake cha TPL kwa Bohari ya Dawa Tanzania (MSD).
Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi ni wafanyakazi wa kiwanda hicho Mkurugenzi Uendeshaji, Seif Shamte, Meneja Masoko, Simon Msoffe na Mhasibu Msaidizi, Fatma Shango, pamoja na wafanyakazi wa MSD, Meneja Udhibiti Ubora, Sadick Materu na Ofisa Udhibiti Ubora, Evans Mwemezi.
Inadaiwa Aprili 5 mwaka 2011, Madabida, Shamte, Msoffe na Fatma walisambazia MSD makopo 12,252 ya dawa bandia za Antiretroviral, ikionesha zimetengenezwa Machi 2011 na mwisho wa matumizi Februari mwaka jana pia walijipatia Sh milioni 148.35 kwa madai ni malipo halali ya dawa hizo.
Materu na Mwemezi wanadaiwa, kati ya Aprili 5 na 13, 2011, Dar es Salaam, wakiwa waajiriwa wa MSD, kwa nia ya kutenda kosa la kusambaza dawa hizo, walishindwa kutumia uwezo wao wote kuzuia kutendeka kwa kosa hilo.
Katika mashitaka mengine, washitakiwa wote wanadaiwa kati ya Aprili 5 na 30, mwaka 2011, kwa nia ovu au sababu za kutotekeleza majukumu yao vizuri, walisababishia MSD hasara ya kiasi hicho cha fedha, kutokana na kuwasambazia dawa bandia.

No comments: