WAZIRI AKERWA NA MAUAJI YA WANAWAKE MKOANI MARA



Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba amesema mauaji ya wanawake katika mkoa wa Mara yanalitia taifa aibu na uvunjaji wa sheria na haki za binadamu.
Alisema hayo jana wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya Siku ya Familia yaliyofanyika mjini hapa.
Alisema kwa mwaka 2014 mauaji ya wanawake mkoani  Mara  yanalitia taifa aibu na kutaka vyombo vya habari kusaidia kuelimisha jamii ili kila mwanajamii aweze kuishi kwa amani na utulivu.
Pia alisema maadhimisho ya siku ya familia yanakumbusha kutafakari jinsi ya kutatua changamoto za malezi ya watoto .
“Siku hizi wazazi na walezi wanawaacha watoto wao kulelewa na wasaidizi wa kazi majumbani, marafiki au walimu shuleni bila kufuatilia mienendo yao kwa kisingizio cha kazi nyingi na hivyo kutokuwa na muda wa kukaa na familia zao,” alisema.
Alisema hata pale wazazi wanapokaa na watoto wao hawana mbinu stahiki za malezi bora kiasi cha kusababisha watoto wao kuiga kile wanachokiona au kusikia kutoka kwa wenzao, shuleni, wanakocheza au wasaidizi majumbani.
Alisema taarifa ya ukatili dhidi ya watoto uliofanyika hapa nchini kati ya mwaka 2009 hadi 2010 ulionesha kuwa ukatili dhidi ya watoto ni wa aina tatu wa kingono, kimwili na kihisia na mara nyingine watoto hukabiliwa na aina zote tatu za ukatili.
Aidha utafiti huo ulionesha kiwango cha ukatili hapa Tanzania ni kikubwa na cha kutisha, vitendo hivyo vinafanyika katika ngazi ya familia ambapo wazazi, walezi na ndugu wa karibu pamoja na walimu ndio wahusika wakuu.
Alisema takwimu zinaonesha asilimia 30 ya wasichana na asilimia 14 ya wavulana walifanyiwa ukatili wa kingono na ndugu, wakati asilimia 80 ya wasichana na asilimia 65 ya wavulana walifanyiwa ukatili wa kihisia kabla ya kufikisha umri wa miaka 18.
Simba alisema familia ni msingi wa Taifa lolote duniani ni vyema mipango imara na ushirikiano wa kutosha unahitajika miongoni mwa wanafamilia, viongozi na wataalam waliopo katika ngazi ya jamii ili kulinda maadili na kuelimisha umuhimu wa malezi bora kwa watoto hasa katika kipindi cha ukuaji.
Aidha akizindua kampeni ya kupiga vita ukatili wa kingono, alisema pamoja na serikali kufanya juhudi mbalimbali za kutokomeza ukatili wa kijinsia bado matukio ya ukatili yanaongezeka.
“Hapa Tanzania takwimu zinaonesha kuwa theluthi moja ya wanawake walio na umri kati ya miaka 15 hadi 49 wamefanyiwa ukatili wa kijinsia na wenzi wao au ndugu zao,” alisema.

No comments: