SHULE YA SEKONDARI AZANIA YAHITAJI VYOO


Shule ya Sekondari Azania jijini Dar es Salaam inaomba msaada wa kukarabatiwa miundombinu ya vyoo, kutokana na miundombinu iliyopo kufungwa kwa kuwa hafifu huku ikiepushwa kutiririsha maji machafu nje ya shule.
Naibu Mkuu wa shule hiyo, Elizabeth Ngoda, alisema hayo jana Dar es salaam wakati akipokea msaada wa kompyuta 10 kutoka  Benki ya Access zenye thamani ya Sh milioni mbili. 
Kuhusu miundombinu shuleni hapo, alisema shule ina wanafunzi zaidi ya 2,000  ambapo  vyoo vinavyotumika havitoshelezi kutokana na vilivyopo kujengwa wakati wa ukoloni, huku idadi ya wanafunzi ikiongezeka mwaka hadi mwaka. 
Alisema shule hiyo imechakaa na inahitaji kukarabatiwa na kutokana na kutitirisha uchafu, husababisha kuwepo kwa harufu kali katika mandhari ya shule hiyo na kuziomba taasisi malimbali kuisaidia kukarabati.
Kuhusu msaada wa kompyuta alisema ni moja ya msisitizo wa matumizi ya Teknolojia ya habari (Tehama)  katika mashule mbalimbali nchini na itasaidia wanafunzi kujiboresha katika eneo hilo.
Alisema shule hiyo ina kompyuta 25 zinazohitaji kuwasaidia wanafunzi wote ambao ni zaidi ya 2,000 huku walimu wakiwa 115 wakitegemea vifaa hivyo pia kwani  karne ya 21  matumizi ya teknolojia ni muhimu  kwa jamii nzima 
“Kompyuta ni  kifaa muhimu ambacho kinahitajika katika maisha ya kila siku ya jamii, ingawaje tunaweza kuwa na idadi chache kwa ajili ya wanafunzi hazitoshi kutokana na iddai yao kuongezeka kila mwaka,” alisema Elizabeth.
Akizungumza, Ofisa Mwandamizi wa Masoko wa Access Bank, Jonas Muganyizi alisema msaada huo ni mpango wao wa kushirikiana na jamii katika faida waipatayo na kuirudisha kwa jamii.
Alisema walianzisha mkakati endelevu wa kugawa kompyuta kwa  shule mbalimbali nchini, lengo likiwa ni kuimarisha matumizi ya kompyuta kwa vijana.
Kwa mujibu wa Muganyizi, benki hiyo tayari ilishatoa vifaa hivyo kwa shule ya sekondari King’ongo iliyopo Kimara, Tuangoma ya Kigamboni, Mchanganyiko iliyopo Ilala na Mugabe.

No comments: