KATIBU MKUU UWT AMTETEA MAMA SALMA KIKWETE


Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Amina Makilagi amesema si sawa kumshutumu Mke wa Rais Mama Salma Kikwete kuwa alitumia nafasi aliyonayo kama Mwenyekiti wa Shirika lisilo la Kiserikali la Wanawake na Maendeleo (WAMA) kumfanyika kampeni mgombea wa CCM, Jakaya Kikwete kwenye uchaguzi mkuu uliopita. 
Kauli ya Makilagi ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum (CCM), imekuja baada ya msemaji wa kambi ya upinzani kwa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Salum Barwany (CUF) kuitaka Serikali kueleza  hatua iliyochukua  dhidi ya WAMA ambayo Mwenyekiti wake ni Mama  Salma. 
Alisema  WAMA ilituhumiwa ndani ya Bunge Aprili mwaka 2012 kuwa ilitumiwa kisiasa na Mama Salma kwenye kampeni za uchaguzi za mwaka 2010 kwa lengo la kumsaidia aliyekuwa mgombea wa CCM wakati huo, Jakaya Kikwete. 
“Tuhuma hizo hazikuwa za kweli, Mama Salma alifanya kazi yake. Suala la wanawake kufanya kampeni halina upinzani huwezi kugombea bila kufanyiwa kampeni kwani hata viongozi wengine wamekuwa wakifanyiwa kampeni na wake zao,” alisema Makilagi. 
Makilagi alisema hawajawahi kupokea  tuhuma dhidi ya WAMA na ni muhimu Salma Kikwete kupongezwa zaidi kwa kazi zake kupitia taasisi ya WAMA. 
“Mimi ni mwanzilishi wa Baraza la Wanawake Tanzania (BAWATA) lilikuwa wazo la UWT tulikubaliana kupitia uongozi wa UWT kuwa na chombo kitakachounganisha wanawake, jambo hilo lilikuwa mahakamani na limetolewa maamuzi na kama mtu anataka ufafanuzi atapatiwa,” alisema. 
Hata hivyo Mbunge wa Mbinga, John Komba (CCM), alisema hakuna jambo la ajabu Mama Kikwete kuzunguka kufanya kampeni kwani ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC). “Kwani wengine wanazunguka na wachumba tu wakimaliza usiku kazi tu, Mama Kikwete ni Mjumbe wa NEC hakuna cha ajabu kufanya hivyo, huo ni ufinyu tu wa fikra,” alisema na kuongeza “Sijui anaitwa Josephine sijui anaitwa nani,” alisema Komba. 
Awali Barwany alisema kutokana na majibu ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba bungeni ya mwaka 2012  kuhusu madai hayo kutoridhisha, mwongozo uliombwa kwa spika kuwezesha hatua kuchukuliwa dhidi yake lakini mpaka sasa muongozo huo haujatolewa majibu.

No comments: