MBUNGE ATAKA UFAFANUZI WACHIMBAJI TANZANITE


Mbunge wa  Simanjiro, Christopher ole Sendeka ameitaka Wizara ya Nishati na Madini kupitia waziri wake, Sospeter Muhongo  kutoa ufafanuzi wa kina juu ya kuondolewa kwa wachimbaji wadogo wa madini ya tanzanite waliopo mpakani, kwa madai wanachimba madini eneo la TanzaniteOne. 
Aidha  baadhi ya wachimbaji hao  walioko mpakani waliitwa na kamishna msaidizi Kanda ya Kaskazini Alex Magayane, na kuwaagiza kuondoa miundombinu yao kwani wanachimba madini kwenye eneo la TanzaniteOne na kutishiwa kufutiwa leseni wasipofanya hivyo. 
Hata hivyo, walipinga amri iliyotolewa na wizara hiyo ya kusitisha uchimbaji wa madini ndani ya kitalu C  kinachopakana na TanzaniteOne, ambapo aliahidi kushughulikia masuala hayo bungeni na kuhakikisha wananchi wanapata haki zao za msingi kulingana na sheria zilizopo. 
Aidha mbunge huyo  aliitaka wizara hiyo kupitia kwa waziri wake Muhongo kutoa ufafanuzi wa kina na sheria waliyoitumia kuwataka wafanyabiashara hao kuondoka katika eneo hilo kwani huo ni uonevu mkubwa ambao haupaswi kuvumiliwa. 
Aidha, Sendeka aliitaka wizara kuacha mara moja utaratibu wa kusitisha leseni za wachimbaji wadogo kwani kufanya hivyo ni uonevu mkubwa ambao kamwe hautaweza kuvumiliwa na wadau mbalimbali wa madini . 
Naye Katibu wa Marema Tawi la Mirerani, Abubakari Madiwa alisema kuwa malalamiko hayo wameshayatoa zaidi ya mara tatu kwa mbunge huyo na viongozi mbalimbali wa madini bila kupatiwa ufumbuzi wowote ambapo walimwomba mbunge huyo kwa mara nyingine tena kushughulikia malalamiko hayo ambayo yameleta athari kubwa kwa wachimbaji wadogo wa madini.

No comments: