IOM KUREJESHA MAKWAO WAHAMIAJI HARAMU


Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) limesema linatarajia  kurudisha wahamiaji haramu 115 walioingia nchini kutokea Ethiopia mwishoni mwa wiki ijayo.
Ofisa Mwendeshaji wa Taifa wa shirika hilo, Charles Mkude,  alisema hayo juzi jijini Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa habari. 
Alisema wamefanya hivyo kupitia mikakati miwili iliyowekwa na serikali ya Japan na Marekani kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa. 
Kwa mujibu wa Mkude, mwaka 2013,  zaidi ya wahamiaji 160,000 waliingia nchini na Afrika Kusini kupitia Kaskazini  mwa Saud Arabia. 
Alisema  wameamua kusaidia wahamiaji hao kurudi nchini kwao kwa kushirikiana na serikali zao. 
 ‘’ Wafanyakazi wote wa IOM, Uhamiaji, maofisa wa Magereza  na maofisa kutoka Ethiopia nao watashiriki kusaidia katika safari yao, ’’alisema Mkude.
Aliongeza kuwa wahamiaji waliokamatwa walifungwa katika magereza mbalimbali yakiwemo ya Pwani, Iringa, Mbeya, Morogoro na Tanga.
Aidha,  kati ya watu 220 walikamatwa wakiwa wadogo, hivyo IOM itawasaidia  masuala yote ya  usafiri  kwani hawana taarifa zozote za kusafiri.
‘’Tumehamasika kuwasaidia kwani  watu hawa wanaishi katika mazingira hatari kwakuwa hawajui  kuongea Kiswahili na hawana ndugu yeyote hapa nchini, pia  Serikali haina pesa za kutosha kuwasafirisha’’ aliongeza.
Awali , alisema kwa kipindi kirefu  Tanzania imekuwa na ongezeko la wahamiaji haramu kutoka pembe ya Afrika hasa Ethiopia na Somalia kutokana na matatizo ya vita ya wenyewe kwa wenyewe.

No comments: