DARASA LA SABA KUFANYA TENA MATOKEO MAKUBWA SASA


Wanafunzi wa Darasa la Saba waliofanya mtihani wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) wakiwa darasa la sita,  watafanya mtihani mwingine wa aina hiyo kabla ya kufanya mtihani wa  mwisho wa kumaliza elimu ya msingi mwaka huu kwa lengo la kuongeza ufaulu.
Kaimu Mkurugenzi wa Elimu ya Msingi, Sarah Mlaki alisema hayo jana wakati akielezea mikakati ya Programu ya BRN katika elimu ya msingi  kuongeza ufaulu na kupunguza wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi bila kujua kusoma na kuandika.
Alisema awali wanafunzi hao walifanya mtihani katika muhula wa pili kwa masomo ya Hisabati Kiswahili na Kiingereza Novemba mwaka jana na sasa watafanya tena awamu ya pili ili kumudu masomo yao vizuri .
Alisema ingawa kuna changamoto ya ukosefu wa fedha katika kutunga mtihani wa BRN  lakini mtihani huo unatarajia kufanyika mapema iwezekanavyo.
Alisema katika mtihani wa sasa wataangalia iwapo wanafunzi wameelewa yale ambayo yalionekana katika mtihani wa kwanza ikiwa ni pamoja na mada ambazo walifeli sana na walimu kupewa mbinu za ufundishaji.
Alisema katika kukabiliana na hali hiyo, wameandaa miongozo ya masomo ya Hisabati, Kiswahili na Kiingereza na itakamilika Julai mwaka huu, kutoa mafunzo kwa wawezeshaji 18 wa ngazi ya Taifa kwa ajili ya kuwafundisha walimu mahiri wa masomo hayo katika ngazi ya Halmashauri.
“Tumefanya uteuzi wa walimu 600 mahiri wa masomo hayo ambao ni 15 toka kila halmashauri kwa halmashauri zote 40 ambao watawafundisha walimu wa shule za msingi kwa mwaka wa fedha ujao,” alisema. 
Mlaki alisema pia wataendesha mitihani ya majaribio ili kuwabaini wnafunzi wenye mahitaji ya ziada katika kujifunza, kufanya uchambuzi wa maswali yenye changamoto kwa wanafunzi kuelewa na walimu katika kujifunza na kutoa mafunzo ya ziada kwa wanafunzi hao.

No comments: