HUYU NDIYE KINARA WA WIZI KWENYE MABENKI


Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limefanikiwa kubaini mtuhumiwa kinara wa wizi wa mabenki, Ronald Mollel (37), ambaye ni mume wa Meneja wa Benki ya Barclays tawi la Kinondoni, Alune Kasililika, anayeshikiliwa na jeshi hilo.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu, Suleiman Kova (pichani), alitoa madai hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu matukio ya ujambazi.
Alisema Mollel  ni  makazi wa Kimara Bonyokwa na taarifa za kuaminika zinadai amekuwa akipanga njama na kushiriki kikamilifu matukio mbalimbali ya uhalifu na kupora mabenki.
Alidai mtuhumiwa huyo ana mtandao na watumishi muhimu katika matawi  ya benki kwa lengo la kufanikisha uhalifu katika benki hizo.
‘’Jeshi la Polisi tumeamua kuweka picha ya  mtuhumiwa huyo hadharani kwa kutumia dhana ya ulinzi shirikishi, ili akionekana akamatwe na taarifa zitolewe katika kituo chochote cha Polisi,’’ alisema Kova.
Pia alisema wamekamata watu watatu kwa tuhuma za ujambazi wakiwa na silaha mbili aina ya Shotgun na risasi 12, Rediocall na sare za Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Alitaja watuhumiwa hao kuwa ni Isihaka Salehe, Alex Andrew na Odinga Swalehe  ambao walikamatwa maeneo ya Chamanzi katika Mkoa wa Kipolisi wa Temeke.
Pia alisema jeshi hilo, limefanikiwa kuufumua mtandao unaojihusisha na ujambazi jijini Dar es Salaam, ikiwemo uvunjaji na kupora nyumba za ibada.
Alisema operesheni hiyo ilianza April 29 mwaka huu, walikamata majambazi sugu wawili nao wakawataja wenzao 13.
‘’Watuhumiwa waliokamatwa katika mtandao mzima ni Shaban Mafuru (36), mkazi wa Magomeni, Abdallah Hussein (52) mkazi wa Tabata Mawenzi, walikutwa kwenye gari namba T259ADB,  ’’ alisema.
Aidha jeshi hilo limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa wawili wakiwa na meno 25 ya kiboko na mmoja akiwa na vipande nane vya meno ya tembo.

No comments: