MWANAFUNZI WA CHUO KIKUU AUAWA KWA KUDAIWA MWIZI



Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT) cha jijini hapa, Helma Michael (22)  ameuawa kwa kupigwa mawe na wanafunzi wenzake, wakimhisi kuwa ni mwizi wa kompyuta ndogo za mkononi na deki chuoni hapo. 
Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Valentino Mlowola, alisema jana kuwa mwanafunzi huyo aliuawa Mei 13 mwaka huu saa 4.00 usiku, katika eneo la Nyamalango Malimbe, ambapo baada ya kubainika katika eneo hilo alianza kupigwa kwa mawe, fimbo na mapanga hadi kusababisha kifo chake.
“Huyu ameuawa katika tuhuma ambazo mpaka sasa hazijathibitishwa,” alisema.  
Kutokana na mauaji hayo, watu 17 wamekamatwa na Polisi  imeanza uchunguzi kuhusu tukio hilo huku Kamanda Mlowola akiwataka watu kutojichukulia sheria mkononi kwa kuwaua watu ambao hawana hatia.
Katika tukio jingine, Kamanda Mlowola alisema mkazi wa Kijiji cha Bugula Kata ya Bwiro wilayani Ukerewe, Bazil Amran aliuawa kwa kupigwa na kipande cha ubao kichwani na Parapara Paulo (36)  kwa tuhuma za wizi. 
Kwa mujibu wa Kamanda Mlowola, mauaji hayo yalitokea Mei 12 mwaka huu saa 11 alfajiri  kijijini hapo ambapo alisema mtuhumiwa amekamatwa na anatarajiwa kufikishwa mahakamani muda wowote kuanzia sasa.
Aidha katika tukio jingine, Kamanda Mlowola alisema Mei 13 mwaka huu majira ya saa saba mchana katika eneo la Mkuyuni kata ya Mahina wilayani Nyamagana, askari polisi waliokuwa doria waliwakamata Sylvesta Musa (31) na Noela Joseph (34) wote wakiwa ni wakazi wa Mkuyuni wakiwa na bastola aina ya LOCK NO. TZ CAR 91968 ikiwa na risasi tano kwenye magazinie yake.

No comments: