HOMA YA DENGUE YAZUA TAFRANI KWA MADEREVA TEKSI DAR



Taarifa isiyo sahihi ya maambukizi ya homa ya dengue inayoenezwa na mbu aina ya aedes, imesababisha baadhi ya madereva teksi jijini Dar es Salaam, kujilinda kwa kuvaa glovu za mikononi, soksi ndefu miguuni na kujifungia muda wote katika magari yao hata ambayo hayana viyoyozi. 
Uchunguzi wa gazeti hili wiki hii, umebaini madereva hao  wamekuwa wakivaa soksi miguuni hata kama wamevaa kandambili, huku wakiwa na glovu viganjani kwa madai kuwa wanaogopa kuumwa na mbu mwenye virusi hivyo.
Wakizungumza na mwandishi, baadhi ya madereva wa kituo cha mtaa wa Mindu  Upanga, walikiri kuvaa mavazi hayo kujikinga  na ugonjwa huo ambao hauna tiba.
“Kwa kweli ugonjwa huu ni hatari kama hauna tiba , unafikiri tutapona kweli, ni heri tuvae hivi, au tujifungie ndani ya gari wakati tunasubiri wateja,” alisema Juma Hassan mmoja wa madereva teksi hao.
Hassan alimruhusu mwandishi kuzungumza naye akiwa amejifungia ndani ya gari huku jasho likimtoka na kulowanisha shati lake, kwa hofu kwamba akifungua madirisha, mbu wataingia na kumwambukiza ugonjwa huo.
Baraka Joseph dereva teksi wa kituo hicho, yeye alikuwa amevaa koti na miguuni amevaa soksi pamoja na kandambili, na alisema taarifa alizonazo zinaonesha ugonjwa huo unatisha kwani unaua muda mfupi na hauna tiba, hivyo sio ugonjwa wa kuudharau hata kidogo.
“Ugonjwa huu unatisha na tumesikia hapa mjini watu wengi wameupata, sasa kazi yetu hii tuko vijiweni tangu alfajiri hadi muda huu (saa mbili usiku), ni lazima tujikinge vinginevyo tutautapa na hatujui kama tutapona,” alisema Joseph.
Hali kwenye kituo cha kona ya Muhimbili, ambako taksi huwa zinapaki hapo, ilikuwa tofauti ambapo kulikuwa na dereva mmoja tu, ambaye naye alisema wenzake wameondoka kwa kuwa maeneo hayo kuna mbu wengi wanahofu ya kuumwa na kupata homa ya dengue.
“Nimebaki mimi ,lakini hata hivyo naondoka, nimejipaka dawa ya kuzuia mbu ila bado nina wasiwasi huenda  mbu mwenye virusi hivyo akaniuma nikaupata, sasa itakuwa shida, kwa kweli ugonjwa huo unatutisha,” alisema Rashid Muhammed, ambaye ni dereva wa teksi eneo la Kona ya Muhimbili.
Wakati huo huo, Mkoa wa Shinyanga ulijikuta ukilazimika kukanusha uvumi ulioenea  kuhusu kulipuka kwa ugonjwa wa dengue, baada ya kulazwa kwa mgonjwa mmoja mwenye viashiria vya ugonjwa huo katika hospitali ya mkoa.
Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake mjini hapa jana Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga, Dk Ntuli Kapologwe, alikanusha kulipuka kwa ugonjwa huo mkoani hapa, baada ya vipimo vya mgonjwa huyo vilivyopelekwa Dar es Salaam, kubaini hana ugonjwa huo.
“Ni kweli mtoto aliyelazwa katika hospitali ya mkoa alikuwa na viashiria vya kuambukizwa ugonjwa huo  vya  uchovu, kuishiwa nguvu, kutokwa na damu puani na homa kali, lakini hakuwa na ugonjwa wa dengue kwa kuwa vipimo vyake kuonesha  anasumbuliwa na ugonjwa mwingine ambao unatibika kwa tiba sahihi,” alisema Dk Kapologwe.
Uvumi kuhusu kuibuka kwa ugonjwa huo, ulisababisha  mkanganyiko uliowakumba baadhi ya wagonjwa  waliofikia hatua ya kutaka kukimbia wadini ili kunusuru maisha yao wakihofia kuambukizwa ugonjwa huo. 
Dk Kapologwe alisema, ili kuthibitisha kuwa mgonjwa aliyefika hospitali kupatiwa matibabu anasumbuliwa na maradhi ya dengue, ni lazima vipimo vyake vipelekwe kwenye Maabara Kuu jijini Dar es Salaam na majibu ya vipimo yathibitishe kuwa kweli mgonjwa huyo ameambukizwa ugonjwa huo. 
Akizungumzia kinga ya ugonjwa huo, Dk Kapologwe aliwataka wananchi kuchukua tahadhari kwa kuchoma na kuangamiza mazingira yanayoweza kuwa chanzo cha mazalia ya mbu ambao husababisha ugonjwa huo.  

No comments: