HOMA YA DENGUE YATINGA MWANZA, MMOJA ALAZWA SEKOU TOURE



Mgonjwa mmoja mkoani hapa, amethibitika kuugua ugonjwa wa dengue na kulazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza ya  Sekou Toure.
Hayo yalibainishwa jana na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Baraka Konisaga katika mkutano wake na waandishi wa habari, uliofanyika jijini hapa kufuatia kuwepo kwa taarifa za mgonjwa huyo.
“Napenda wananchi wa Mkoa wa Mwanza, watambue kuwepo kwa ugonjwa wa dengue na kwamba hadi sasa mgonjwa mmoja amethibitika kuugua na amelazwa tangu jana (juzi),” alisema.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Valentine Bangi alisema mgonjwa huyo, ambaye ni mtumishi wa serikali mstaafu (bila kutaja jina lake) na mkazi wa Kilimahewa, alifika hospitalini kwa mara ya kwanza Mei 20, mwaka huu.
Alisema alifanyiwa vipimo, lakini siku iliyofuata alirudi na kusema hali yake sio nzuri na ndipo walipoamua kuchukua vipimo vya dengue.
 Alisema Mkoa umepokea vipimo 50 vya ugonjwa wa dengue, ambapo 10 wamevisambaza  katika Wilaya ya Kwimba, 10 Wilaya ya Ukerewe na 10 wilayani Sengerema.
Alisema Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii itapeleka vitendanishi vingine kwa sababu hivyo vilivyopo, walivipokea kabla ya kuwepo kwa ugonjwa huo mkoani hapa.
Ugonjwa huo huambukizwa na virusi, wanaotokana na mbu aina ya Aedes, baada ya kumng’ata mtu mwenye ugonjwa huo na kisha kumng'ata mtu mwingine.
Asilimia 90 ya wagonjwa walioambukizwa, huonesha dalili ndani ya siku tatu hadi 14. Dalili hizo ni homa kali, kichwa kuuma machoni, kichefuchefu, kutapika, kuvimba tezi, maumivu makali ya viungo na kupatwa na harara.
Hivi karibuni, Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Kebwe S. Kebwe alisema mabadiliko ya tabianchi na mwingiliano wa safari, vimesababisha kuwepo kwa ugonjwa wa dengue, ambao ulianzia kwenye nchi za Asia.

No comments: