ATCL YAREJESHA SAFARI ZAKE ZA ZANZIBAR NA ARUSHA



Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL) imerejesha safari zake katika anga za Arusha na Zanzibar  na kuahidi kusafiri katika maeneo hayo yenye vivutio bora vya kiutalii mara sita kwa wiki.
Katika safari hiyo ya uzinduzi ya kutoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar kupitia Arusha, iliyofanyika jana,  kulikuwa na mawaziri wawili wa pande zote za Muungano .  ATCL itakuwa ikitumia ndege yake aina ya Bombardier Dash - 8 yenye uwezo wa kubeba abiria 50 katika njia hiyo.
Ikitokea Dar es Salaam kwenda Arusha, alikuwemo Waziri wa Maliasili na Utalii Lazaro Nyalandu na wakati wa kutoka Zanzibar kwenda Dar es Salaam, alipanda Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais (Utawala Bora) wa Serikali ya Zanzibar, Dk Mwinyihaji  Haji Makame. 
Akizungumza mara baada ya kutua katika uwanja wa ndege wa Arusha, Nyalandu alisema kurejea kwa ndege za ATCL katika njia ya Arusha na Zanzibar, kutakuza sekta ya utalii na kurahisisha uunganishwaji wa maeneo hayo muhimu yenye vivutio vikubwa vya utalii.
“Uzinduzi wa safari hii unadhihirisha kwamba sasa ushindani wa kweli katika sekta ya usafiri wa anga umeanza. ATCL inatakiwa kuhakikisha inaendeleza dhamira yake ya kutoa huduma bora ili iweze kurejesha imani iliyokuwanayo kwa abiria wake walio wengi,” alisema Nyalandu.
Kaimu Mkurugenzi wa Biashara wa ATCL, Juma Boma alisema safari ya Dar es Salaam – Arusha – Zanzibar ni sehemu ya mkakati wa shirika lake kutanua huduma katika maeneo mengi iwezekanavyo.
“Tunajivunia kuendelea kutekeleza dhamira yetu ya kuimarisha huduma zetu tukiwa kama kampuni  ya ndege la taifa. Tukilenga kuendelea kutanua wigo wa huduma zetu ndani ya nchi na kimataifa. Lengo letu kubwa ni kuendelea kutoa huduma zenye gharama nafuu, vile vile kuongeza uwezo wa abiria kusafiri kwa wakati wao,” alisema. 
Alisema wameondoa adhabu kwa  abiria wanaochelewa kufika uwanja wa ndege au kushindwa kufika siku ya safari na wanaobadilisha tarehe za safari zao. 
Waziri Makame alisema inatia moyo kuona ATCL ikirejesha safari zake Zanzibar baada ya kusitisha huduma zake katika  kisiwa hicho kwa zaidi ya miaka minne. 
Alitaka ATCL kufuata muda na kuhakikisha wanapunguza adha ya usitishaji wa safari endapo wanataka kurejesha imani miongoni mwa abiria walio wengi.
Akizungumza baada ya kupokea safari hiyo ya uzinduzi katika uwanja wa ndege wa Arusha, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, John Mongela alisema kuanza kwa safari  katika Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki , kumerejesha sifa iliyokuwa nayo ndege hiyo ya taifa kipindi cha nyuma wakati wa mikutano ya kimataifa jijini Arusha. 

No comments: