HIVI NDIVYO WAGENI WANAVYOPORA AJIRA ZA WATANZANIA



Uwepo wa vyombo mbalimbali vinavyotoa kibali cha kufanya kazi nchini, umetoa mwanya kwa wageni kuingia nchini na kuajiriwa katika nafasi za kazi, ambazo baadhi hata Watanzania wana uwezo wa kuzijaza. 
Mwishoni mwa wiki iliyopita wakati wa  Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi), Rais Jakaya Kikwete alisema Serikali imebaini kuwa tatizo hilo la kutolewa kwa vibali kiholela, linatokana na vibali hivyo, kutolewa na taasisi zaidi ya moja.
Mwandishi amepata taarifa kutoka Wizara ya Kazi na Ajira, inayoonesha namna wafanyakazi hao, wanavyopata vibali vya kufanya kazi nchini, jambo lililolalamikiwa na wafanyakazi kuwa baadhi ya wageni hao, wanapata ajira ambazo Watanzania wanaweza kuzijaza kwa ufanisi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, vibali vya kufanya kazi nchini kwa wageni, vimekuwa vikitolewa na Wizara ya Kazi na Ajira, kupitia Kamati ya Utatu inayoundwa na Wizara, Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta) na  Chama cha Waajiri nchini (ATE).
Hata hivyo, baada ya mgeni kukubaliwa kupata kibali na Wizara kupitia utatu huo, wageni hao hupata kibali kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Idara ya Uhamiaji ambacho ni kibali Daraja B, kinachoruhusu wageni watakaoajiriwa kwa masharti ya kudumu tu.
Mbali na Wizara ya Kazi na Ajira, taarifa hiyo imeeleza kuwa vibali Daraja A na C, hutolewa moja kwa moja na Idara ya Uhamiaji, bila kupitia Wizara hiyo.
ÒIdara ya Uhamiaji pia ina mamlaka pia ya kutoa vibali vya muda mfupi bila kupitia Wizara ya Kazi na Ajira, mfano vibali vya miezi mitatu mpaka sita kwa wageni ambao wanakuja kufanya kazi kwa muda mfupi,Ó imeeleza taarifa hiyo.
Utaratibu unaotumiwa na Wizara ya Kazi na Ajira, kutoa kibali kwa mgeni kufanya kazi nchini, kwa kushirikisha ATE na Tucta, huzingatia mambo mbalimbali.
Kwanza taarifa hiyo imeeleza kuwa kibali hukubaliwa kwa kuzingatia idadi ya miradi, ambayo kampuni husika inayo na muda ambao miradi hiyo itakamilika.
Pia, kabla ya kutoa kibali, mapendekezo ya wizara zenye dhamana ya kupendekeza waombaji huzingatiwa, mfano Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa upande wa walimu, Wizara ya Ujenzi kwa wageni katika miradi ya ujenzi na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, sababu nyingine inayozingatiwa wakati wa utoaji kibali katika Wizara ya Kazi na Ajira, imetajwa kuwa ni cheo cha muombaji, ukubwa wa kampuni na idadi ya Watanzania, walioajiriwa na kampuni husika.
Mamlaka nyingine inayohusika kutoa vibali vya ajira kwa wageni ni Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC).
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Sheria ya Uwekezaji ya 1997 Ibara ya 24 (1) (2), inaruhusu waombaji watano wa mwanzo katika mradi wa uwekezaji, wapewe vibali vya kufanya kazi nchini, hata kama sifa zao Watanzania wanazo.
Mbali na waombaji hao watano wa mwanzo, Sheria hiyo imewaruhusu pia wawekezaji, kuongeza wageni zaidi ya hao watano katika ajira wanazotoa, kulingana na umuhimu wa mtu wanayemuombea.
Nafasi zao, watokako
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uchambuzi uliofanyika wizarani, umeonesha wageni wengi wanaokuja kufanya kazi nchini, hupendelea nafasi za umeneja, ambazo ndizo zenye malipo mazuri.
"Uchambuzi unaonesha mameneja (uendeshaji, masoko, fedha na kadhalika), ndio wanaoongoza kwa idadi ya wageni wanaokuja kufanya kazi nchini," taarifa hiyo  imeeleza.
Wengine ni wataalamu, ambao hawako katika mchanganuo wa kisekta, wakiwemo mafundi mchundo katika sekta ya ujenzi, walimu, wasimamizi, mameneja wakuu na wakurugenzi, wafanyakazi katika viwanda vya chuma, wahandisi na wanasayansi.
Nchi zinazoongoza kwa kuwa na wingi wa wageni wanaofanya kazi nchini, kwa mujibu wa taarifa hiyo, ni India ikifuatiwa na China, Kenya, Afrika Kusini, Pakistani na Uingereza.
Taarifa hiyo imekiri kuwa kumekuwa na udanganyifu mkubwa kwa wanaopewa vibali hivyo, ambapo baadhi ya wawekezaji wanapata vibali na kufanya kazi, ambazo  hazipo katika vibali vyao.
"Wafanyabiashara ndogo hasa maduka, hawapendekezwi kupewa vibali isipokuwa kumekuwa kukifanyika udanganyifu mkubwa, mfano wanaingia nchini kama wawekezaji na nyaraka zote muhimu wanapata na wakipewa hawafanyi lengo lililowaleta.
"Wizara ya Viwanda na Biashara,  Msajili wa Makampuni (Brela) na TIC kubaini mbinu zote na kuchukua hatua kwa kuwa ili mtu afanye biashara hapa nchini, taasisi mbalimbali zinahusika," ilieleza taarifa hiyo.
Akizungumza mwishoni mwa wiki katika sherehe za Mei Mosi, zilizofanyika kitaifa jijini Dar es Salaam, Rais Kikwete alisema kutokana na kukithiri kwa malalamiko ya Watanzania, kuhusu kutolewa holela kwa vibali vya kazi kwa wageni, Serikali inafikiria kurekebisha Sheria ya Vibali vya Ajira kwa Wageni, ili kudhibiti ipasavyo utolewaji wa vibali hivyo.
Alisema Serikali imebaini kuwa tatizo hilo la kutolewa kwa vibali kiholela, linatokana na vibali hivyo kutolewa na taasisi zaidi ya moja.
"Hali hii inatoa fursa kwa watumishi wasio waaminifu kutumia mwanya huo wa taasisi nyingi kuidhinisha vibali hivi na kuvitoa hata kwa watu wasiostahili kwa kujinufaisha, hili hatuwezi kulinyamazia," alisema Rais Kikwete.
Alisema kutokana na kukithiri kwa tatizo hilo, Serikali imekuwa ikipokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi, juu ya kujaa kwa wageni nchini, wanaofanyakazi hata zile zinazoweza kufanywa na wananchi wa kawaida, jambo linalowanyima ajira wananchi wengi.
Aliwaahidi Watanzania kuwa Serikali imeliona tatizo hilo na iko kwenye mchakato wa kulifanyia kazi kwa kuipitia upya Sheria hiyo na kuandaa muswada wa marekebisho katika kipengele cha vibali vya ajira kwa wageni.
Alisema moja ya mapendekezo, yanayofanyiwa kazi kwa ajili ya kurekebishwa katika sheria hiyo, ni pamoja na eneo la taasisi zinazohusika kutoa vibali hivyo, ambapo katika marekebisho hayo, itapendekezwa iwe taasisi moja pekee.
"Tutarekebisha na kutoa fursa ya kutoa vibali hivyo kwa taasisi moja pekee na kuiongezea udhibiti, ili endapo kutatokea wafanyakazi wasio waaminifu iwe rahisi kuwabaini na kuwadhibiti," alisisitiza.

No comments: