KINANA SASA AMTAKA MAALIM SEIF AACHIE NGAZI



Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimemtaka Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Seif Sharif Hamad, kama kweli hataki Muungano wa serikali mbili, amuandikie barua  Rais wa Zanzibar, Dk Mohamed Shein na kujiuzulu wadhifa wake wa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.
Tamko hilo lilitolewa jana na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, wakati akihutubia mkutano mkubwa wa hadhara, uliofanyika kwenye viwanja vya Kibandamaiti mjini Unguja.
Kinana alisema anachokifanya Seif ni sawa na kuwaramba vichogo wanasiasa wenzake wa upinzani, wakati yeye akipata mshahara na marupurupu mengine, yanayomwendeshea maisha yake chini ya serikali ya CCM.
Alisema kama kweli Maalim Seif anajigamba ni jasiri, achukue uamuzi sahihi wa kujiuzulu wadhifa wake, ili apate nafasi ya kutosha kuwatumikia wananchi nje ya Serikali.
Kinana alieleza kuwa kutembea nchi nzima kwa Seif, si kitendo cha uungwana kufanywa na kiongozi mwenye wadhifa wa Makamu wa Kwanza wa Rais, akiwa ndani ya Serikali inayomlipa mshahara na huduma nyingine muhimu, akaamua kuwachochea wenzake, ambao wako nje ya Serikali kuleta chokochoko dhidi ya Serikali anayoitumikia.  
Maalim Seif ameshatuhumiwa kuwa kigeugeu katika maisha yake ya kisiasa, ambapo hivi karibuni Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Mohammed Seif Khatib, alielezea namna kiongozi huyo wa CUF, alivyowahi kuwa mtetezi wa serikali mbili alipokuwa kiongozi katika Serikali ya CCM, ambako alitumia nguvu kubwa kupinga vuguvugu la kudai serikali tatu mwaka 1984.
Khatibu alinukuu kauli ya Maalim Seif alipokuwa akipambana na watu, waliokuwa wakitaka serikali tatu, akiwepo Rais wa Zanzibar wa wakati huo, Aboud Jumbe.
"Msimamo wa Jumbe umetufadhaisha sisi sote, tunataka maelezo yake kwa kuwa ni dhahiri hoja ya serikali tatu haikuanzishwa na watu wadogo, imechangiwa pia na baadhi ya viongozi wa Baraza la Mapinduzi na Aboud Jumbe ni chanzo cha hayo," alinukuliwa Maalim Seif akisema mwaka 1984.
Viongozi ambao Maalim Seif alikuwa akisema wanataka serikali tatu na kwa kufanya hivyo wamemfadhaisha na wanastahili adhabu pamoja na Jumbe ni  Jamal Faki, Abuu Salim na Wolfgang Dourado, ambaye alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Kwanza wa Zanzibar.
"Tuangalie viongozi wanaobadilika badilikaƉmwaka 1984 Maalim Seif alitaka serikali mbili, mwaka 1992 akiwa CUF msimamo wake ukawa serikali tatu, juzi serikali ya mkataba, huyu ni kiongozi wa aina gani? Ni wa kuongopea watu tu," alisema Khatibu.
Kinana katika mkutano wa jana aliendelea kusema: "Maalim Seif aache kuwababaisha wananchi, atulie kwa sababu ameamua kutumikia serikali za CCM na hana uwezo wowote wa kuvuruga amani ya Taifa kama anavyojigamba kwenye majukwaa ya kisiasa."
Aliongeza kuwa Katibu Mkuu huyo wa CUF, anaposimama na kutaka muundo wa Muungano wa serikali tatu, hiyo ni danganya toto, lakini kila mwenye macho na masikio, anatambua nia ya kiongozi huyo ni kutaka kuusambaratisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa maslahi yake na rafiki zake.
Kinana alisema Tanganyika kukosa Serikali wakati Zanzibar ikiwa na mamlaka ya ndani si kioja, kwani hata Uingereza yenye Muungano wa nchi za Wales, Scotland, Ireland ya Kaskazini na England, ina kiti kimoja Umoja wa Mataifa. Pia, alisema England ambako anatoka Malkia Elizabeth II, haina Serikali.
Kwa upande wake, Mnadhimu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Salmin Awadh Salmin, alisema wawakilishi wa CCM wanatazamia kuwasilisha hoja binafsi kwenye Baraza la Wawakilishi Zanzibar, ili wananchi waulizwe kama wanaafiki mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa visiwani humo au la.
Salmin alisema dhamira na madhumuni ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, imefutika na haileti tena matumaini kwa wananchi, kwa kuwa pande mbili za kisiasa, zinazounda ushirika huo, zina itikadi zinazotofautiana.
"Tutawasilisha hoja binafsi Baraza la Wawakilishi, ili wananchi wapige kura ya maoni kama wanaafiki muundo huo au hawautaki, CCM haitakubali kufanya kazi na watu wenye itikadi, mitazamo na misimamo tofauti, wenzetu ni adui wa Muungano na Mapinduzi Zanzibar," alisema Salmin.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Dk Emmanuel Nchimbi, aliwaeleza wananchi kwamba hakuna mahali ambapo Rais Jakaya Kikwete, alisema majeshi yatachukua nchi, kama inavyoenezwa kwa uongo na wapinzani kwa makusudi.
Dk Nchimbi alifafanua kuwa Rais Kikwete alisema kukiwa na Muungano wa serikali tatu na ile ya Muungano ikiwa haina vyanzo vya uhakika vya mapato, kuna hatari ya Jeshi kuchukua madaraka ikiwa wanajeshi watashindwa kulipwa mishahara yao kwa wakati na kwa uhakika.
"Kinachofanywa na wapinzani ni kutapatapa kwa kukosa hoja, wasimlishe maneno Rais ambayo hajayasema, waseme alivyosema na kama wana hoja wajibu kwa nguvu ya hoja na si hoja dhaifu na upotoshaji unaoendelea," alisema Dk Nchimbi.
Akizungumzia kuhusu Muungano, alitoa mfano wa Taifa la Marekani, lenye Muungano wa nchi zaidi ya 50, ambapo katika miaka 47 ya Muungano, taifa hilo lilipata misukosuko, lakini halikuyumba na mpaka sasa limebaki kuwa taifa moja lenye kiti kimoja katika Umoja wa Mataifa.
Alisema nchi nyingine zote katika Taifa hilo, zina mamlaka ya ndani na hakuna Mmarekani hata mmoja, anayefikiria au kutamani kusambaratika kwa Taifa hilo lenye nguvu zaidi kiuchumi duniani.
Katika hatua nyingine, Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wamehadharishwa na tabia ya  Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif, kwa kuwa   ni mwanasiasa kigeugeu, anayeweza kuwasaliti na kuwatosa wakati wowote.
Katibu wa Idara ya Oganaizesheni ya CCM, Seif Khatib, alisema hayo wakati akihutubia mkutano wa hadhara katika uwanja wa Kibandamaiti mjini Unguja, Zanzibar.
Khatib alisema Umoja huo, hautafika mahali popote, kwani mmoja kati ya wanachama wa umoja huo, ambaye ni Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif, atawatosa kama alivyomtosa aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Aboud Jumbe.
Alitaja viongozi wengine waliowahi kutoswa na Maalim Seif  mwaka 1984 kuwa ni Waziri Kiongozi wa zamani, Ramadhan Haji Faki na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar,  Wolfang Dourado.
Alisema anawashangaa  viongozi wa vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi, DP na NLD kukubali kushirikiana na kiongozi huyo, mwenye sifa na historia ya kusaliti wanasiasa wenziwe na viongozi wa kiserikali katika maisha yake.
"Alimsaliti Jumbe mwaka 1984, akamtosa James Mapalala mwaka 1994, akachongea kina Naila Jidawi na Shaibu Akwilombe na mwisho amemzamisha Hamad Rashid Mohamed, Ukawa iko siku watajuta kumsikiliza kiongozi huyo," alisema Khatib.
Aidha, Mwanasiasa huyo mkongwe na Waziri wa zamani wa Muungano, aliwaeleza wananchi kwamba kitendo cha kiongozi huyo, kuwashinikiza wajumbe wa Bunge la Katiba, wasusie vikao vya Bunge Maalum wakati yeye akiwa Makamo wa Kwanza wa Rais, ni aina ya usaliti wa kisiasa.
Kwa upande mwingine, Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde, aliwaasa wananchi wa Zanzibar, kumpuuza Maalim Seif na badala yake waendelee kudumisha amani, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na kuyalinda Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.
"Nje ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Mapinduzi ya Zanzibar yatapotea, amani, umoja wa kitaifa na mshikamano vitapotea, ni jukumu la kila mmoja kukataa uchochezi wa aina yoyote, unaoenezwa na wapinzani nchini," alisema Khatib.

No comments: