Baraza la Madiwani la Hamashauri ya Wilaya ya Mwanga, limeunda
kamati ya watu watano ili kumuona Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama,
kujua sababu za kuwapo mgomo wa vyombo vya dola katika kudhibiti uvuvi haramu
katika Bwawa la Nyumba ya Mungu.
Kamati hiyo itaongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi, Ujenzi na
Mazingira, Kuria Rajabu na itakuwa na wajumbe Enea Mrutu, Kilavo Mndeme,
Mohamed Mgala na Sofia Sharokiwa. Itaanza kazi mara moja kunusuru kutoweka kwa samaki katika bwawa
hilo.
Kamati hiyo itakuwa huru na itakuwa na jukumu la kutafuta chanzo
cha mgomo huo waliouita baridi, licha ya Halmashauri kutenga Sh milioni 100 katika bajeti yake ya
mwaka 2013/2014, ambazo hazijatumika hadi sasa.
Akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri
hiyo, Mrutu ambaye ni Diwani wa Kata ya
Shighatini, alisema anashangazwa na kutotumika kwa fedha hizo, licha ya kwamba
uvuvi haramu unaendelea kwa kasi.
Hofu ya Baraza iliyosababisha kuundwa kwa kamati hiyo, inatokana na
taarifa ya Kamati ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira, kuelezea changamoto
zinazowakabili, ikiwa ni pamoja na kushindwa kuanza kwa operesheni hiyo baada
ya kukosa ushirikiano na Jeshi la Polisi.
Awali, akiwasilisha taarifa
ya Kamati yake, Kuria alisema fedha hizo zilitengwa kwa ajili ya semina na
operesheni ya kuzuia uvuvi haramu na kwamba katika operesheni zilizopita,
wananchi waliharibu magari ya Polisi.
Hata hivyo akizungumza kwa simu, Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Shaibu
Ndemanga, alisema vyombo vya dola havijagoma kushiriki operesheni hiyo, bali
kilichotakiwa kufanywa ni ushirikishwaji wa wanajamii wenyewe, badala ya
kutanguliza nguvu za polisi.
Alisema maelekezo yaliyotolewa ni kutaka kufahamu mipango ya
halmashauri, baadaye kama itaonekana
kuna vurugu, ndipo Polisi itatumika
kuhakikisha usalama unakuwepo, badala ya kuwatumia sasa, ambapo inaweza
kuonekana mabavu zaidi yanatumika.
Alisema iwapo polisi watahitajika kulingana na hali halisi,
watakwenda katika operesheni hiyo na kuongeza kuwa siku za nyuma kulitokea
uvumi, uliosababisha magari ya Polisi kuvunjwa vioo na wananchi wanaojiita
wenye hasira.
Kutokana na taarifa hiyo, Mrutu alilieleza baraza hilo kuwa huenda
matokeo ya operesheni zilizopita, ndiyo sababu zilizosababisha polisi kususia
kushiriki operesheni nyingine za halmashauri hiyo, ingawa alisema kamati
iliyoundwa, itatoa jibu kamili.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo,Theresia Msuya
alithibitisha kuwapo kwa mgomo huo,
aliosema aliuthibitisha kupitia taarifa aliyopewa na Mkuu wa Wilaya ya
Mwanga, kuwa Polisi inataka wanajamii wenyewe washiriki operesheni hiyo.
Alisema mgomo huo, umeifanya Wilaya ya Mwanga kuomba msaada wa
Polisi kutoka Mkoa wa Tanga, ambao hata hivyo hawajaupata, kwa madai bado
Polisi mkoani Kilimanjaro, haijatoa kibali kwa Polisi Mkoa wa Tanga kutoa
msaada, kama zilivyo taratibu za jeshi
No comments:
Post a Comment