EU YAZUNGUMZIA MATUNDA YA OPERESHENI ZA MAJESHI YAKE


Umoja wa nchi za Ulaya (EU) umeingia makubaliano na nchi zilizo ukanda wa bahari ya Hindi ikiwemo Tanzania kwa ajili ya kuzuia uharamia.
Mwakilishi wa umoja wa nchi za Ulaya (EU), Tom Vens aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuwa makubaliano hayo yameshazaa matunda kwa kupungua kwa kasi ya utekaji nyara meli.
Amesema EU inashirikiana na Tanzania katika mambo mengi, ikiwa ni pamoja na kuondoa uharamia katika bahari ya Hindi.
Hata hivyo, Kamanda wa Jeshi la Wanamaji la EU, Jurgen zur Muhlen alisema katika kipindi kifupi walichofanya kazi katika bahari ya Hindi changamoto kubwa waliyokumbana nayo ni nani haramia na nani ni mtu salama.
Alisema wametoa mafunzo mbalimbali kwa jeshi la wanamaji hapa nchini namna ya kukamata wahalifu majini, kupata na kutunza vielelezo na pia uendeshaji wa kesi za uharamia majini.
Hata hivyo alisema mbali na ulinzi huo kupunguza kwa kiasi kikubwa uharamia baharini hasa kwa Somalia, hakuna watu waliofikishwa mahakamani isipokuwa kushikiliwa kwa uchunguzi.
Meja Anton Mkaliha ambaye ni mratibu katika msafara huo wa jeshi la EU, alisema ujio wa jeshi hilo umeonesha mafanikio makubwa mpaka sasa kwani kwa kiwango kikubwa uhalifu unadhibitiwa. 

"Kipindi cha nyuma tulikuwa tukisikia uhalifu ukifanyika katika bahari ya Hindi lakini sasa hali hiyo haisikiki tena kutokana na ulinzi unaofanywa na manuari hizi za jeshi la EU," alisema Meja Mkaliha.

No comments: