VYAMA VYA SIASA VYAANZA MJADALA KUONDOA MAKUNDI


Viongozi wa vyama vya siasa nchini wameanza kujadili namna ya kuondoa makundi katika Bunge maalumu la Katiba kwa njia ya mazungumzo, yakielezwa ndivyo yanayosababisha migogoro iliyopo.
 Aidha, wataangalia namna ya kufanya mazungumzo ya malalamiko kwa kila kundi wakiwa nje ya bunge hilo maalumu linalotarajiwa kuanza tena Agosti 5, mwaka huu baada ya Rais Jakaya Kikwete kuliongezea siku 60, baada ya siku 70 za awali kuishia `juu juu’. 
Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Peter Mziray aliyasema hayo jana katika kikao maalumu cha baraza hilo kujadili mustakabali wa Bunge Maalumu la Katiba baada ya kundi linalojiita Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kutoka nje ya ukumbi wa bunge na kusisitiza kutorejea. 
Katika kikao hicho kilichoshirikisha viongozi wa vyama hivyo, walianza kwa kujadili hotuba ya Rais Kikwete aliyoitoa Februari mwaka huu alipozungumza na viongozi hao kabla ya kuanza kwa bunge hilo.
Katika hotuba yake, Rais alieleza kuwa inapotokea majadiliano katika Bunge Maalumu la Katiba yanapokuwa magumu au kutokuelewana ni vema kukaa pamoja na kutafuta mwafaka, hivyo kwa kuzingatia msingi huo wa Rais, wamekutana ili kila upande kutoa malalamiko yake na kuangalia namna ya kufikia mwafaka ikiwezekana hata kuwatafuta watu wanaoheshimika katika jamii na kusaidia kufikia muafaka. 
“Mnakumbuka mgogoro wa vyama vya CUF na CCM Zanzibar, ulimalizika kwa njia ya mazungumzo kwa kila upande kukubali kueleza dukuduku zake na kusikilizana ndivyo tunavyotaka kufanya sasa,” alisema.
Mziray alisema ni wazi kuwa makundi yanayosababisha migogoro kwenye bunge hilo ni wanasiasa hivyo kama baraza lazima kutafuta ufumbuzi wa tatizo lililopo sasa katika bunge hilo kwa muda huu nje ya bunge kwani muda bado upo.
Mwenyekiti  wa Chama cha United People's Democratic Party (UPDP), Fahmi Dovutwa, alisema ili kufikia muafaka wa tatizo lililopo bungeni ni kila upande kukubali kusikiliza wengine na kuondoa jazba.
Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Philip Mangula alisema ni vema kutumia ushauri wa Rais kufikia mwafaka wa jambo hilo kwa kukaa na kutafuta ufumbuzi kwa kujadiliana.
Huku Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima Tanzania (AFP), Said Soud Said akitaka Rais Kikwete kukaa na viongozi wa vyama vya siasa kuzungumza nao kwa kuwapa nafasi kusikiliza kwani ni  dhahiri anapenda mabadiliko.

No comments: