DODOMA WATENGA MILIONI 500/- KUTOA MOTISHA KWA WALIMUMkoa wa Dodoma umetenga Sh milioni 500 katika bajeti yake ya Mkoa kwa mwaka ujao wa fedha, kwa ajili ya kutoa motisha kwa shule, waalimu na wanafunzi watakaofanya vizuri katika mitihani ya kuhitimu elimu ya msingi na sekondari.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Rehema Nchimbi alisema hayo katika Uwanja wa Jamhuri mjini hapa katika salamu zake za makaribisho kwenye Maonesho ya Wiki ya Elimu.
Alisema hayo mbele ya Waziri Mkuu, Mizengo  Pinda, aliyekuwa mgeni rasmi.
Aliishukuru Serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kwa kuupa heshima kubwa Mkoa wa Dodoma kuwa mwenyeji wa maonesho hayo kitaifa.
Alitaja  maendeleo mazuri yaliyofikiwa kielimu mkoani hapa tangu kuzinduliwa kwa Mpango wa Taifa wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) kuwa ni waalimu wengi kujiendeleza kielimu kutoka daraja moja kwenda jingine la juu kitaaluma, na baadhi yao kujiunga na Chuo Kikuu Huria  cha Tanzania (OUT), wakisoma huku wakiwa kazini.
Alisema Mkoa huo umefanya marekebisho kwenye baadhi ya sera zake za ndani ili kuendana na Mpango wa Matokea Makubwa Sasa ili kujenga  mazingira rafiki ya kutoa matokea ya elimu kwa haraka.
Alieleza kuwa ofisi yake, imefanya makubaliano na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ili mahafali yajayo ya wahitimu wake, yafanyike kitaifa Dodoma ili Mkoa uweze kutoa tuzo za wahitimu wa kozi za Ualimu, watakaohitimu kutoka chuo hicho na pia yawe yakifanyika rasmi mkoani hapa.

No comments: