MFUKO WA MKOBA WAWA KIMBILIO LA WAJASIRIAMALIMfuko wa Mitaji ya Wafanyabiashara (Mkoba Private Equity Fund), uliozinduliwa na Rais Jakaya Kikwete hivi karibuni, umeelezwa kuwa ndio kimbilio kubwa kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati katika kupata mitaji ya kukuza biashara zao.
Balozi wa Heshima wa Botswana Tanzania,  Emmanuel ole Naiko, ameuelezea mfuko huo kuwa kimbilio la wajasiriamali.
"Uzinduzi wa mfuko huo umekuja wakati mwafaka kwa vile Tanzania tuna tatizo kwa wajasiriamali wadogo na wakati kupata mitaji ya kuendeleza na kukuza shughuli zao za kibiashara," alisema Ole Naiko mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam wakati akifungua semina ya siku moja ya wajasiriamali wa Asasi ya Diana Women Empowerment Organization.
Alisema Serikali kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), imejitahidi kuweka mifumo mizuri ya sheria kwa ajili ya wawekezaji wa ndani na nje, lakini tatizo lililopo ni namna ya kupata mitaji kwa vile benki zina masharti magumu ya kupata mikopo.
"Kwa kweli uzinduzi wa mfuko huo utachochea shughuli za biashara na ujasiriamali hapa nchini kwa vile kutakuwa na sehemu ya kupata mitaji," alisema na kuongeza kuwa ni vyema wajasiriamali wachangamkie fursa za kuwepo kwa mfuko huo.
Ole Naiko ambaye pia ni mlezi wa asasi hiyo, aliwaasa pia wanasemina hao kuzingatia mafunzo ya ujasiriamali na kwamba elimu, mbinu na maarifaƊ wanayoyapata wayatumie kwa vitendo ili kuzidi kuendelea kibiashara.
"Mafanikio katika biashara yanaanza kwa mtu mwenyewe na hakuna mtu anayeweza kuja kuwaendeleza katika biashara zenu bila wenyewe kujitambua na kujiongezea maarifa," alisema.
Aliwaasa wajasiriamali hao kuzitumia fursa zinazojitokeza za kupata mikopo kwa ajili ya kukuza biashara kwa faida yao na Taifa kwa ujumla, kwani mchango wa wajasiriamali ni mkubwa sana.
Mwenyekiti wa Taifa wa Asasi hiyo, Farida Khakoo alisema semina hiyo ilishirikisha wajasiriamali 40 ambao ni wanachama wa asasi hiyo.
"Asasi yetu inalea watoto yatima, walemavu na wajane na ina wanachama ambao ni wajasiriamali," alisema.
Alisema semina hiyo inalenga kuwafundisha namna ya kutunza kumbukumbu za hesabu za biashara zao katika vitabu ili waendeshe vema biashara.
Mwanachama na mjasiriamali wa asasi hiyo, Constance Chandende, alisema semina hiyo itamwezesha kupata ujuzi zaidi wa kuendesha shughuli zake za ujasiriamali na kufikia malengo.
"Mimi biashara yangu ni ya kusindika matunda yakiwemo ya pilipili mbuzi, michaichai, maembe na mbilimbi," alisema.
Alisema wanawake wengine nchini wasikae bila kazi bali wajiingize katika biashara mbalimbali ili waweze kuwa na mchango katika familia.

No comments: