SEKONDARI YA NAMFUA YAGEUZWA KUWA CHUO CHA WALIMU



Jumuiya ya  Wazazi mkoani Kilimanjaro imefanya mabadiliko ya Shule yake ya Sekondari Namfua wilayani Rombo na kuigeuza  Chuo cha Ualimu.
Chuo hicho kitaitwa Chuo cha Ualimu cha Mkoa wa Kilimanjaro na kinatarajia kupokea wanafunzi kuanzia Julai, mwaka huu.
Mbali na Sekondari ya Namfua,  pia jumuiya hiyo imeifunga Shule ya Sekondari Kahe wilayani Moshi,   tayari kwa ajili ya maandalizi ya kuanza  kuwa Chuo cha Kilimo. Hata hivyo, bado michakato haijaanza na sasa wanatafuta fedha.
Mwenyekiti wa  Jumuiya hiyo mkoani hapa, Festo Kilawe  alisema tayari wanafunzi waliokuwa wakisoma Namfua, wamehamishiwa shule nyingine za jumuiya mkoani humo kwa ajili ya maandalizi ya kupokea wanafunzi wa Ualimu ili kukabili upungufu wa walimu nchini.
Kilawe alisema shule hiyo iliyokuwa na wanafunzi zaidi ya 150, wamehamishiwa katika Shule za Kibo wilayani Moshi na  Mwanga na Minja wilayani Mwanga.
Walimu wa shule hiyo, nao wamehamishiwa katika shule hizo, walizokwenda wanafunzi hao.
"Jumuiya ina shule 11 mkoani hapa, tumekaa tukakubaliana kwamba idadi ya shule za sekondari tulizonazo ukichanganya na shule za kata ni nyingi mno...mfano Rombo pekee ina shule za sekondari 48, tumeona upungufu uliopo sasa ni vyuo," alisema.
Kilawe alisema ukarabati wa Shule ya Namfua iliyopo Kata ya Nanjararea Tarafa ya Tarakea ili kuwa Chuo cha Ualimu, umegharimu zaidi ya Sh milioni 200, zilizotolewa na jumuiya hiyo ngazi ya Taifa, ikiwamo Sh milioni 80 kutoka jumuiya hiyo mkoani Kilimanjaro.
Alisema wameteua Shule ya Namfua, kutokana na kuwa na ekari 30 za ardhi ambazo zinatosha kwa ajili ya upanuzi wa chuo hicho, ambacho kitakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,800 wa cheti cha ualimu  na diploma ya ualimu kwa mwaka.
Kuhusu Shule ya Kahe, Mwenyekiti huyo alisema mipango ya kufungua Chuo cha Kilimo ipo katika hatua nzuri, kwani lengo la jumuiya hiyo ngazi ya taifa ni kubadili mfumo wa elimu uliopo sasa, ikiwezekana hata kufungua chuo kikuu cha jumuiya hiyo.

No comments: