DARAJA LA WAMI KUJENGWA UPYA



Wizara ya Ujenzi imetangaza kujenga daraja jipya la Wami mkoani Pwani, ambalo ni kiungo kikubwa katika usafiri wa barabara kati ya mikoa ya Kaskazini mwa Tanzania na nchi jirani.
Waziri Dk John Magufuli alitangaza hayo juzi usiku, wakati akiwasilisha bungeni makadirio ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2014/15, na kueleza kuwa Sh milioni 300 zimetengwa kwa ajili ya mradi huo katika mwaka ujao wa fedha.
“Lengo la mradi huu ni kujenga daraja jipya katika Mto Wami kwenye Barabara ya Chalinze – Segera, ili kuboresha usalama katika daraja hilo.
Katika mwaka wa fedha 2014/15, Sh 300 zimetengwa kwa ajili ya kuanza upembuzi yakinifu na usanifu wa kina pamoja na utayarishaji wa nyaraka za zabuni,” Dk Magufuli alilieleza  akiomba Bunge limuidhinishie bajeti ya Sh trilioni 1.22. 
Akizungumzia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa mwaka 2013/14, Dk Magufuli  alisema wizara iliidhinishiwa na Bunge Sh bilioni 845.12 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, na kati ya hizo, Sh bilioni 604.4 zilitolewa hadi Aprili, 2014 sawa na asilimia 71.52. 
Kuhusu barabara, alisema miradi mingi imetengewa fedha ukiwamo Mradi wa Mabasi ya Haraka Dar es Salaam (DART), pamoja na barabara zake za pembezoni, ambazo zitajengwa kwa kiwango cha lami ili kupunguza tatizo kubwa la msongamano jijini humo. 
Akielezea mradi huo, alisema unahusisha ujenzi wa barabara kutoka Kimara hadi Kivukoni yenye urefu wa kilometa 15.8 kwenye Barabara ya Morogoro, Barabara ya Kawawa kutoka Magomeni hadi Morocco kilometa 3.4 na Barabara ya Msimbazi kutoka Fire hadi Kariakoo kilometa 1.7. 
Akitoa mchanganuo wa barabara za mikoa, alisema zimetengewa Sh bilioni 31.9, ambazo kazi zake zitakuwa   ukarabati kwa kiwango cha changarawe, kujenga kwa kiwango cha lami na kujenga madaraja katika mikoa yote ya Tanzania Bara. 
Alisema kazi zilizopangwa kutekelezwa kwa upande wa barabara za mikoa  ni ukarabati wa kilometa 685 kwa   changarawe, kujenga kilometa 78 kwa lami na ujenzi wa madaraja 14. Aidha, upembuzi yakinifu utaendelea kwa barabara zenye urefu wa kilometa 1,520.50. 
Kwa mujibu wa waziri, Tanzania ina mtandao wa barabara zenye urefu wa jumla ya kilometa 87,581 kati ya hizo, kilometa 35,000 ni Barabara Kuu na za Mikoa zinazosimamiwa na Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala wa Barabara (Tanroads). 
“Kilometa 52,581 zilizobaki ni barabara za Wilaya na zinasimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu Tamisemi kupitia Mamlaka za Serikali za Mitaa. Aidha, kuna jumla ya madaraja 4,880 katika Barabara Kuu na Barabara za Mikoa,” alisema Dk Magufuli ambaye jana jioni Bunge lilitarajiwa kuidhinisha bajeti yake. 
Katika taarifa yake, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, ilishauri Serikali ipitie upya mikataba ya nyumba zilizouzwa kwa watumishi wa umma, ili kubaini nyumba zilizobadilishwa matumizi ambazo hazitumiki kama makazi kama ilivyokusudiwa, ili zitakazobainika kukiuka mikataba ya kuuziwa nyumba hizo, zirudishwe serikalini.

No comments: