Wasomi wa Chuo
Kikuu cha Mtakatifu Augustino (Saut), wamemualika aliyekuwa Waziri Mkuu,
Fredrick Sumaye mkoani Kagera, kwenda kutoa mihadhara kwa wasomi na
watu wa kada mbali mbali katika mkoa huo.
Mwaliko huo
umetokana na mihadhara aliyotoa katika vyuo vikuu mbali mbali nchini Marekani
hivi, ambayo iliwagusa kiasi cha kuamua kufanya Kongamano kuchambua mada mbalimbali alizotoa kiongozi huyo.
Taarifa ya
wasomi hao iliyotumwa jana kwa vyombo vya habari, ilieleza kuwa wasomi hao
wameamua kuendelea kuchambua hotuba hizo kwa kuoanisha na mazingira ya sasa ya
Tanzania na Bara la Afrika.
Pia
walikubaliana watumie wigo na wasomi wenzao wa vyuo mbalimbali hapa nchini, ili
kupata mawazo zaidi kwa faida ya
Watanzania.
Wasomi hao
wapatao 189 wanatoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (Saut), Kampasi ya
Bukoba, Tumaini University na shule za
sekondari za Ihungo, Rugambwa, Nyakato na Kahororo.
Sumaye alikuwa
nchini Marekani kwa karibu mwezi mmoja
na alirejea nchini Aprili mwaka huu.
Akiwa huko alipata nafasi ya kutoka mihadhara katika Chuo Kikuu cha Wellesley
Boston, Morehouse College Atlanta George (USA), Elizabeth State
University North Caroline (USA), na
Havard University katika 20th Annual International Conference Day.
Mada iliyokuwa
na mjadala mkali ilikua ni kuhusu viongozi wengi wa Afrika kutokuwa na moyo wa
uzalendo na hasa kujitumbukiza katika
rushwa kubwa kubwa, kujilimbikizia
mali na kuficha fedha katika
mabenki ya Ulaya huku bara la Afrika likiendelea kuwa masikini.
Pia wasomi hao
walijadili kuhusu hali ya elimu duni isiyoendana na dunia ya leo, vifo vya
watoto na wajawazito, miundombinu hafifu, vita ya wenyewe kwa wenyewe na
matatizo mengi yanayoikabili bara la Afrika.
Kuhusu suala la
haki za binadamu wasomi walikubaliana kuwa umefika wakati sasa wa nchi za
kiafrika kuchukua hatua za haraka kuhakikisha kuwa watu wote wanapata haki zao
za msingi bila kubaguliwa hasa katika masuala ya elimu, chakula, afya, haki za
kupata habari.
Kuhusu Afrika
kushiriki katika uchumi wa dunia walikubaliana na Sumaye kuwa umefika wakati bara la Afrika
lisiangaliwe kama chimbuko la rasilimali tu bali kama mbia na mshirika mkubwa
katika uchumi wa dunia kwa kuwa lina
rasilimali kubwa ya ardhi yenye rutuba, madini, maji na hata rasilimali watu.
Pia suala la waafrika kujitambua
ni jambo lililojitokeza kwenye mada za wasomi hao.
No comments:
Post a Comment