CLOUDS MEDIA KURUSHA MATANGAZO YAKE UARABUNI


Kampuni ya Clouds Media International  imepatiwa leseni ya kurusha  matangazo  katika nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni  hiyo inayomiliki Clouds Radio na Clouds Tv, Joseph Kusaga ilisema kuwa kwa sasa Clouds TV International imekuwa ya kimataifa na itakuwa ikishuhudiwa na watu wa mataifa mbalimbali.
"Clouds TV kimataifa ni mwendelezo wa televisheni maarufu sana kwa vijana  nchini Tanzania,  hata hivyo sehemu kubwa ya maudhui yatakayokuwemo kwenye Clouds TV kimataifa itakuwa na mpangilio mpana wa vipindi kwa watazamaji vitakavyorushwa kwa  lugha za Kiingereza na Kifaransa,” alisema Kusaga.
Kusaga aliongeza kuwa "Leo ni siku ya  kihistoria na alama ya hatua moja katika mpango wetu wa kina wa kupeleka maudhui ya Clouds TV kimataifa kupitia  matangazo kwa njia ya  mitandao.’’
Alisema kuwa Clouds TV kimataifa  haitatoa tu burudani, lakini pia itakuwa kiunganishi kwa Waafrika waishio katika Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu pamoja na kuwapa fursa za kutangaza bidhaa zao na kuimarisha uhusiano baina yao.
Aliongeza kuwa vituo vya televisheni katika Umoja wa Falme za Kiarabu vipo vingi na vyenye ushindani mkubwa, lakini Clouds TV kimataifa imebahatika kupata nafasi ya kurusha matangazo yatakayowafikia walengwa katika chaneli yenye uwezo wa kuwahudumia zaidi ya watazamaji  takribani milioni 3.5 kutoka katika nchi za Afrika. 
“Kwa sasa hakuna kituo kinachotoa huduma hii na hivyo kuwa fursa muhimu kwa watazamaji,” alisema Kusaga.
Alifafanua kuwa Clouds TV kimataifa itarusha vipindi vya burudani, tamthiliya, maigizo, ucheshi, na muziki, vyote vitakavyo kuwa vimeandaliwa kutoka nchi za Mashariki, Magharibi na Kusini mwa bara la Afrika na itapatikana kwa watazamaji walio katika Umoja wa Falme za Kiarabu kupitia huduma ya IPTV inayotolewa  na Etisalat na Du.

No comments: