DK BILAL AWAFUNDA WAFANYABIASHARA NDOGO WA KEMIKALI


Baadhi ya wafanyabiashara ndogo wametajwa  kuchanganya kemikali na vyakula bila utaratibu hali inayodaiwa kuhatarisha afya za walaji wa vyakula hivyo.
Makamu wa Rais, Dk Mohammed Gharib Bilal alisema hayo hivi karibuni jijini Dar es Salaam na kusema taasisi ya saratani ya Ocean Road, imekuwa ikipokea wagonjwa wapya 5,000 wa saratani.
Alisema  tabia na vitendo hivyo vya kuchanganya vyakula na kemikali, si vya kiungwana. Ameahidi kwamba serikali itaendelea kusimamia  na kuhakikisha matumizi sahihi  ya kemikali yanakuwepo. 
Alisema  kemikali zisipotumiwa vizuri, zina madhara makubwa  kwa binadamu ikiwemo kusababisha ongezeko la ugonjwa wa saratani na maradhi mengine. 
Alisema  kemikali hutumika kuzalisha mbolea, dawa za kuulia wadudu, kutengeneza dawa za hospitalini, ujenzi wa nyumba kama saruji, rangi, mbao na mabati na matumizi mengine mengi.
Aidha alisema changamoto kubwa katika hilo ni namna bora na salama ya kutumia kemikali hizo  zisilete madhara kwa afya ya watu na kuziepusha kuingia kwenye mfumo wa ikolojia na kuchafua mazingira.
Hata hivyo alisema madhara ya kemikali yanaweza kuwa ya muda mrefu au mfupi kulingana na kiwango kitakachoingia mwilini. Kemikali zinaweza kuharibu mifumo ya fahamu, damu, uzazi na hata mifupa.

No comments: