MTOTO AFARIKI BAADA YA KUTUMBUKIA KISIMANI


Mtoto wa kiume aliyetambuliwa kwa jina la Yunus Abijan (4) amekufa baada ya kutumbukia katika kisima cha maji kilicho jirani na nyumba yao.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Engelbert Kiondo alisema, tukio hilo ni la juzi saa 8:45 mchana huko maeneo ya Keko Machungwa, Wilaya ya Temeke.
Alisema mtoto huyo alikutwa akiwa ametumbukia katika kisima hicho ambacho hakikuwa na mfuniko kinachomilikiwa na Pili Ally. 
Mtoto huyo alikufa wakati akiwa njiani kupelekwa Hospitali ya Polisi Baracks, maiti amehifadhiwa Hospitali ya Temeke.
Katika tukio jingine, mwendesha pikipiki aliyetambuliwa kwa jina la Athumani Abdallah (28), amekufa baada ya kugongwa na lori.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi, ajali hiyo ni ya juzi saa 5:50 asubuhi katika Makutano ya Barabara ya Tabata na Mandela.
Alisema gari aina ya Leyland Daf lenye namba T936 BNT lenye tela namba T442 AWM ikiendeshwa na mtu asiyefahamika akitoka Ubungo kwenda Buguruni  aligongana na pikipiki yenye namba T237 CPM aina ya Sanya iliyokuwa ikiendeshwa na mtu huyo.
Maiti amehifadhiwa Hospitali ya Amana na jitihada za kumtafuta dereva wa lori aliyekimbia baada ya ajali bado zinaendelea. Gari hilo linashikiliwa na polisi na upelelezi unaendelea.

No comments: