CHAMA KINGINE CHA SIASA CHAPA USAJILI WA KUDUMU



Chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT-Tanzania), jana kilikabidhiwa cheti cha usajili wa kudumu na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi.
Jaji Mutungi alikabidhi cheti hicho mjini Dodoma jana kwa Kaimu Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Kadawi Limbu na kuwataka  viongozi wa chama hicho kufanya siasa zenye ukomavu kwa kuzingatia Sheria ya Vyama vya Siasa. 
Aliwataka viongozi wa chama hicho, kuheshimu wanachama wao kwani vyama vingi vikishapata usajili, viongozi wake wanaanza kujiona wanajua kuliko wanachama wao. 
“Mmepata usajili huku nchi ina amani, fanyeni siasa  zitakazohakikisha nchi inaendelea kuwa na amani,” alisema Jaji Mutungi na kutaka chama hicho kushiriki kutoa maoni kuhusu marekebisho Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria ya Gharama za Uchaguzi.
Msaidizi wa Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza,  alipongeza ACT kwa kutimiza masharti yote ya kupata usajili wa kudumu na kuongeza kuwa chama  hicho kilifanikiwa kupata wanachama zaidi ya 200 katika mikoa 10 ya Tanzania Bara na mikoa miwili kutokea Zanzibar.
Aliwataka viongozi wake kufahamu kwamba sasa wako chini ya Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria ya Gharama za Uchaguzi na kuwataka kuepuka ushindani na vyama vingine unaoweza kusababisha wasahau sheria zinazoongoza vyama vyao.
“Epukeni kujihusisha katika vurugu, Sheria inakataza vyama vya siasa kutumia nguvu katika siasa, hali hiyo inafifisha demokrasia na kuwatia hofu wanachama,” alisema Nyahoza.
Aliwataka kuepuka migogoro ya ndani ya chama chao kwakuwa  mara nyingi vyama vya siasa vinapotafuta, viongozi wake wanakuwa pamoja, wakishapata wengine wanaota mapembe.
Limbu alisema  chama hicho kimepanga kuonesha demokrasia ya kweli nchini na hakitakuwa  chama cha vurugu.
“Chama hiki kitakuwa chama cha heshima, hakitakuwa na mmiliki kitakuwa cha wanachama, hatutegemei migogoro na tutafanya siasa za kistaarabu,” alisema.
Alisema chama hicho kitashiriki kikamilifu kufanyia
maboresho Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria Gharama za Uchaguzi, ikiwemo kuhakikisha Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa inakuwa na meno kwa vyama vya siasa,” alisema Limbu.
Kuhusu chama hicho kuwa na watu maarufu nyuma yake, Limbu alisema hayo ni masuala ya kusikika sio kweli kwani wao ni wanasiasa wazoefu, wanajiamini na hakuna sababu ya kufanya kazi kwa kuwa kuna watu nyuma yao.
“Kuna  watu na viongozi wa vyama vingine wanakerwa na demokrasia ndani ya vyama vyao, vipo vyama ambavyo ni  kampuni ya watu, ukionekana kugusa maslahi ya mtu unafukuzwa tunawakaribisha waje tujenge demokrasia ya kweli,” alisema Limbu.

No comments: